STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 29, 2010

AIBU! Ulimboka anaswa akihonga Mtibwa



WINGA wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya soka, Ulimboka Mwakingwe, alikamatwa na polisi na kulazwa korokoroni juzi kwa tuhuma za kumhonga fedha kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado ili aachie magoli wakati Mtibwa itakapocheza dhidi ya Simba katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro leo jioni.
Ulimboka alinaswa na kisha kutupwa mbaroni katika kituo cha polisi Mtibwa, ikiwa ni muda mfupi baada ya kunaswa kwenye eneo la kambi ya Mtibwa iliyopo Manungu, Turiani Morogoro, akidaiwa kumhonga Kado kiasi cha fedha kinachotajwa kuwa ni Sh. 400,000 ili aiachie Simba katika mechi yao.
Habari zilizoifikia Micharazo jana, zilisema kuwa Ulimboka, winga aliyeng’ara Simba kwa misimu kadhaa kabla ya kuomba apumzike msimu huu, alinaswa kirahisi kufuatia kile kinachodaiwa kuwa ni mtego uliowekwa mapema dhidi yake.
Chanzo kingine kilidai kwamba alikamatwa majira ya saa 2:30 usiku na kupata kashkash za kupewa kipigo baada ya kukutwa na Kado kwenye kota za Mtibwa, na kudaiwa vilevile kwamba alikutwa na fedha zote zinazodaiwa kuwa za hongo.
Alipoulizwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, alithibitisha juu ya kukamatwa kwa Ulimboka kambini kwa timu ya Mtibwa na kwamba kilichomkamatisha ni hizo tuhuma za kumhonga Kado.
Alisema kuwa polisi walimshikilia katika kituo chao cha Mtibwa hadi jana asubuhi kabla ya kumuachia kwa dhamana.
"Ni kweli… taarifa za kukamatwa kwa mchezaji huyo (Ulimboka) ninazo, ila sina uhakika kama alipigwa. Nilichoambiwa ni kwamba alinaswa na fedha na kufikishwa kituoni na watu wa Mtibwa Sugar ambapo alihojiwa, akafunguliwa kesi na kisha kuachiwa asubuhi hii (jana)," alisema Kamanda Andengenye.
Kamanda huyo alisema kuwa pamoja na kuachiwa kwake (Ulimboka), bado jeshi lao linaendelea na upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Awali, kocha msaidizi wa Mtibwa, kipa wa zamani wa Simba, Patrick Mwangata, alikiri pia kutokea kwa tukio hilo kambini kwao, lakini hakutaka kuzungumza zaidi kwavile yeye si msemaji rasmi na kwamba, suala hilo liko mikononi mwa polisi.
Micharazo haikumpata Ulimboka ili aelezee sakata hilo na sababu za kuhusishwa na Simba wakati akiwa ameshaachana nao na kubaki kuwa mchezaji mstaafu wa ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Baadhi ya viongozi wa Simba hawakupatikana pia kupitia simu zao za mikononi, ingawa Afisa Habari wa klabu hiyo, Clifford Ndimbo, alipatikana awali na kuomba apigiwe baada ya dakika kumi, jambo ambalo halikufanikiwa kwani alipopigiwa tena baada ya muda huo kwa zaidi ya mara mbili, simu yake haikuwa ikipatikana.
Wakati Simba na Mtibwa zikishuka dimbani leo, Idda Mushi anaripoti kutoka Morogoro kuwa African Lyon walilazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi yao ya ligi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Kagera walipata goli la utangulizi katika dakika ya 43 kupitia kwa Gaudence Mwaikimba na Lyon wakasawazisha katika dakika ya 54 kwa penati iliyopigwa na Adam Kingwande kufuatia kipa Amani Simba kumdaka miguu Idrisa Rashid na kutolewa kwa kadi nyekundu.
Huku wakiwa 10 uwanjani, Kagera walipata goli la pili katika dakika ya 66 kupitia kwa Sunday Hinju kabla Kingwande tena kuisawazishia Lyon kwa goli la dakika ya 88.

No comments:

Post a Comment