STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 28, 2011

Villa yaapa kufa na Simba, yadai ushamba umeshawatoka




KLABU ya soka ya Villa Squad umedai 'ushamba' waliokuwa nao katika Ligi Kuu Tanzania Bara umeshawatoka na kuionya Simba isitarajie mteremko kwenye pambano lao lijalo.
Simba waliopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo nyuma ya Toto Afrika, itaikaribisha Villa katika pambano litakalochezwa Septemba 8, uwanja wa Mkwakwani, mjini Tanga.
Licha ya uongozi huo wa Villa, kukiri kuwa Simba ni timu nzuri, bado wanaionya kwamba isitarajie wepesi kutokana na kikosi chao kujipanga kuwakabili ili kushinda mchezo huo.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi, alisema mapema leo asubuhi kuwa, kipigo cha mabao 3-0 walichopewa na Toto Afrika katika mechi yao ya awali iliwatoa ushamba na kwa sasa kikosi chao kimeanza kuizoea ligi hiyo na kuonyesha ushindani wa kweli.
Uledi, alisema kuthibitisha hilo waliweza kuibana Kagera Sugar nyumbani kwao na kutoka sare ya bao 1-1 , hali inayowafanya kujiamini wanaweza kuikabili timu yoyote ikiwemo Simba na Yanga.
"Aisee tunaendelea kujiandaa kwa ajili ya pambano letu na Simba, kifupi ni kwamba tumeshaanza kuizoea ligi na kwamba wapinzani wetu wasitarajie mteremko Mkwakwani, hiyo Septmba 8," alisema.
Aliongeza, benchi lao la ufundi linatumia mapumziko ya wiki moja ya ligi kuu kurekebisha matatizo yaliyotokea katika mechi za awali ili kuweza kuingia dimbani kuikabili Simba wakiwa fiti.
"Timu inaendelea kujifua na tuna imani mapumziko yaliyopo yatawapa nafasi makocha na wachezaji kuweka mambo sawa," alisema.
Uledi alisema wachezaji wao wawili waliokuwa majeruhi wameanza kupaata nafuu na kwamba hadi siku ya pambano hilo hali yao itakuwa imetengemaa na kurejea dimbani kuisaidia timu yao.
Klabu hiyo ya Villa Squad inayoshikilia mkia kwa sasa katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi moja, ni miongoni mwa timu nne zilizopanda ligi kuu msimu huu, nyimngine zikiwa ni Coastal Union, JKT Oljoro na Moro United.

Mwisho

No comments:

Post a Comment