STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 28, 2011

Timu ya Ngumi kuondoka leo mchana




TIMU ya taifa ya mchezo wa ngumi itakayoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Michezo ya Afrika (All African Games) inatarajiwa kuondoka mchana huu kuelekea nchini Msumbiji, ikiwa na mabondia wanne pamoja na viongozi wawili.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi Tanzania, BFT, Makore Mashaga, aliiambia MICHARAZO kuwa, timu hiyo imelazimika kuwahia mapema kwenda Maputo, kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya kuanza kwa michuano hiyo kutoka Septemba 3 hadi Septemba 1.
Mashaga, alisema kikosi hicho kilitarajiwa kuondoka jana kwa ndege kikiwa na mabondia wanne na makocha wao wawili tayari kwenda kuwahi zoezi la upimaji afya litakalofanyika kesho (Agosti 30).
"Hapa ninapozungumza nawe nipo katika harakati za kukamilisha kuiwahisha timu uwanja wa ndege ili kuondoka kwenda Msumbiji, ambapo timu yetu itawakilisha na mabondia wanne na makocha wao wawili," alisema Mashaga.
Katibu huyo aliwataja mabondia hao kuwa ni Emilian Patrick atakayepigana uzani wa Feather, Martin Joseph (Middle) na Seleman Kidunda na Macmillian Patrick ambao watapigana uzito wa juu (kilo 91).
"Hao ndio mabondia watakaiwakilisha Tanzania baada ya kufanyika mchujo chini ya makocha, Hurtado Pimenter na msaidizi wake, ambao nao wapo kwenye msafara huo wa kwenda Msumbiji," alisema.
Mashaga alisema BFT ina imani kubwa kwa timu hiyo kufanya vema kama mabondia na makocha wao walivyowaahidi Watanzania kwamba wanaenda kushindana na sio kushiriki au kuwa wasindikizaji.
Mara ya mwisho Tanzania kufanya vema kwenye mashindano hayo kwa upande wa ngumi ilikuwa michuano ya mwaka 2007, yaliyofanyika nchini Algeria ambapo bondia Emilian Patrick aliambulia medali ya fedha.
Wakati huohuo timu ya taifa ya michezo ya Walemavu (Paralimpiki) yenye wachezaji watano inatarajiwa kuondoka Jumatano kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo ya All African Games.
Timu zingine zitakazowakilisha Tanzania katika michezo hiyo ya 10 ya Afrika itakayofanyikia kwenye dimba la Zimpeto, mjini Maputo ni zile za Riadha, Netiboli na Soka ambazo zitaondoka pia Jumatano.

Mwisho

No comments:

Post a Comment