STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 8, 2011

Ubalozi wa UAE wafuturisha waislam Dar

UBALOZI wa Nchi ya Falme za Kiarabu, UAE nchini kupitia taasisi ya kutoa huduma za kijamii ya Khalifa Bin Zaayid Al Nahyaan, umeamua kuwafuturisha waumini wa dini ya kiislam wa Msikiti wa Al Rahman wa Dar es Salaam kwa mwezi mzima wa mfungo wa Ramadhani.
Msaada huo wa futari unaoambatana na tende, ulianzwa kutolewa juzi jioni ambao mamia ya waumini wa msikiti huo walipata fursa ya kufuru chakula hicho kabla ya usiku kugawiwa tende zilizotolewa na ubalozi huo wa UAE.
Imamu wa Msikiti huo wa Al Rahman uliopo eneo la Kinondoni, Sheikh Abdullah Salim Bahssany, akiwahutubia waumini wake wakati wakigawiwa futari hiyo, alisema huo ni msaada toka ubalozi wa UAE na utakuwa ukitolewa hapo kila siku hadi mwezi mtukufu wa Ramadhani utakapomalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Imamu huyo aliwaambia waumini hao kuwa wale waliokuwa na shaka na kupata futari katika funga zao, waondoe hofu kwani sasa watakuwa wakipata chakula hicho, huku akiushukuru ubalozi huo kwa ukarimu iliyouonyesha kwa waumini hao.
"Jamani futari mnayokula leo imetolewa na ubalozi wa nchi za Falme za Kiarabu na msaada huu utakuwa ukitolewa kwa mwezi mzima katika mfungo huu wa Ramadhani hivyo msiwe na hofu katika funga zenu,"alisema Sheikh Bahssany.
Baadhi ya waumini waliofuturishwa msikiti hapo waliushukuru ubalozi huo na kuomba watu wengine wenye uwezo kuiga mfano huo wakidai mwezi huu ndio wa waumini wa kweli kuonyesha upendo, ukarimu na kuhurumiana katika kutekeleza nguzo ya nne kati ya tano za Imani za Kiislam.

Mwisho

No comments:

Post a Comment