STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 8, 2011

Simba Day ni leo Arusha, uhondo wapungua




KUHAMISHWA kwa tamasha la klabu ya Simba, 'Simba Day' kupelekwa jijini Arusha kumevuruga baadhi ya ratiba zilizokuwa zimepangwa, ingawa uongozi umesema kila kitu kipo sawa na kwamba leo watatambulisha rasmi kikosi chao kipya cha msimu huu jijini humo.
Tamasha hilo linalofanyika kwa mwaka wa tatu mfululizo, awali lilipangwa kufanyika jijini Dar es Salaam, lakini limekwama baada ya kukosekana muafaka wa malipo baina ya uongozi wa klabu hiyo na ule unaosimamia uwanja wa Taifa, na kulazimika kupelekwa Sheikh Amri Abeid.
Kutokana na kuhamishwa huko mkoani Arusha, baadhi ya mambo yaliyotarajiwa kufanyika leo kama pambano la timu za vijana za Simba na Azam U20 limefutwa na badala yake itachezwa mechi ya timu ya veterani ya Arusha dhidi ya viongozi wa Simba.
Kadhalika, bendi na vikundi vilivyokuwa vitumbuize katika tamasha hilo, pia vimeshindikana sawa na tukio la utoaji wa tuzo za wadau walioisaidia Simba kwa hali na mali, ambapo kesho watapewa wachache watakaobahatika kwenda jijini Arusha na wengine watatangazwa tu.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliiambia MICHARAZO, kuwa pamoja na hali iliyotokea iliyowatatiza kidogo, kila kitu kinatarajiwa kufanyika kwa ufanisi leo ambapo timu yao itakitambulisha rasmi kikosi chao kipya chenye wachezaji wapya wa kimataifa.
"Ni kweli kuhamishwa kwa tamasha hili toka Dar hadi Arusha kumevuruga baadhi ya mambo, lakini kila kitu kipo sawa na wakazi wa Arusha watarajie burudani ya kutosha kwani mambo yamerekebishwa, ili kufanikisha tamasha hilo," alisema Kamwaga.
Kamwaga, alisema kikosi chao tayari kipo jijini humo tangu Ijumaa kikijifua kabla ya leo kuvaana na Simba ya Uganda iliyotarajiwa kutua jana na kusafiri kwenda Arusha kwa ajili ya mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa.
Alisema kikosi chao kipo kamili ukiondoa Mwinyi Kazimoto anayeendelea kujiuguza majeraha yake aliyopata siku ya mechi ya fainali ya Kombe la Kagame kati ya Simba na Yanga, huku wachezaji wengine wawili, Ulimboka Mwakingwe na Amri Kiemba wakirejea toka majeruhi.
Kamwaga alisema watatumia tamasha hilo na hasa mechi yao na Simba ya Uganda kupima kikosi chao kabla ya kuvaana na Yanga wiki ijayo katika pambano la Ngao ya Jamii ikiwa ni uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana Agosti 17 katika pambano litakalofanyika kwenye uwanja wa Taifa, ikiwa ni wiki kadhaa tangu timu hizo kukutana kwenye fainali hizo za kombe la Kagame na Yanga kuibuka mshindi wa bao 1-0 lililofungwa na Mghana Kenneth Asamoah.

Mwisho

No comments:

Post a Comment