STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 15, 2017

Mwanariadha wa Tanzania, Alphonce Simbu ang'ara India Marathon

Simbu (wa pili kushoto) akipozi na washindani wake baada ya kutwaa nafasi ya kwanza wa Mbio za kimataifa za India Marathon 2017
Na Lasteck Alfred
MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu, ameibuka mshindi kwenye mbio ndefu za Mumbai Marathon  2017, akifanikiwa kumpiku Mkenya Joshua Kipkorir na wakimbiaji wengine wazoefu kutoka mabara mbalimbali.
Mashindano hayo yajulikanayo kama Standard Chartered Mumbai Marathon huwa yanafanyika kila Jumapili ya tatu ya Januari katika jiji la Mumbai, India na yanaaminika kuwa ni mbio kubwa kabisa barani Asia kwa idadi ya washiriki.
Simbu, aliyedhaminiwa na kampuni ya Multichoice Tanzania, aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa dakika 2:09:28 muda ambao ni mzuri sana kwa mbio za aina hiyo.
Akizungumzia ushindi wake, Simbu alisema ushindi huo umesababishwa na maandalizi mazuri aliyoyafanya.
Alisema anauchukulia ushindi huo kama changamoto kwa mashindano mengine makubwa na kwamba huo ni mwanzo tu. Amesisitiza kuwa ushindi huo sio wake pekee yake au Multichoice ambao ndio wathamini wake, bali ni ushindi wa Taifa zima.
Kwa upande wa Serikali,  Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alimpongeza kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema: "Tumefanikiwa tena, hongera Simbu, hongera RT (Chama cha Riadha Tanzania), asanteni Multichoice Tanzania kwa kumsapoti. Mungu ibariki Tanzania."
Kwa upande wake Mkuu wa Mahusiano wa Multichoice Tanzania, Johnson Mshana alisema Multichoice imefurahishwa sana na matokeo hayo na kwamba wataendela kumdhamini Simbu kwa mujibu wa makubaliano yao, ili kuhakikisha anaendelea kufanya vyema na kuliletea taifa sifa kubwa.
“Tulichukua jukumu la kumdhamini simbu katika mazoezi na maandalizi yake kwa kipindi cha mwaka mzima, kwani tunafahamu fika kuwa mazoezi na maandalizi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika mchezo wowote.
Alisema Mshana na kuongeza “Dhamira yetu kubwa ni kuinua vipaji na kulirejesha taifa letu kwenye ramani ya dunia katika ulingo wa michezo na burudani”
Katika mbio hizo, waigizaji maarufu wa Bollywood John Abraham and Neha Dhupia walikuwepo kuleta amsha amsha kwa washiriki. Alphonce anatarajiwa kurejea nyumbani leo Jumatatu.

No comments:

Post a Comment