STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 15, 2017

Breaking News: Mwili wa Amina kuletwa, kuagwa Dar kesho

Na Mwandishi Wetu

HABARI zilizotufikia muda huu, zinasema kuwa mwili wa Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Limited, inayochapisha magazeti ya Uhuru, Uhuru Wikiendi, Burudani na Mzalendo, Amina Athuman unatarajiwa kurejeshwa Dar es Salaam kesho asubuhi kwa boti kutoka Zanzibar. Msemaji wa Familia ya Marehemu, Athumani Kazukamwe, amesema jioni hii kuwa, mwili wa Amina utasafirishwa kutoka Zanzibar saa moja asubuhi kwa boti na unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kati ya saa tatu na saa nne asubuhi.
Kazukamwe, ambaye ni baba mkubwa wa mume wa marehemu, amesema mazishi ya Amina yamepangwa kufanyika keshokutwa Jumanne katika makaburi ya Soni, nje kidogo ya mji wa Tanga.
Amesema awali, upande wa mume wa marehemu ulitaka mazishi hayo yafanyike kesho Dar es Salaam, lakini baada ya majadiliano na familia ya marehemu, waliafikiana mazishi yakafanyika Tanga.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa familia ya marehemu, taratibu za kuuaga mwili wa Amina zitafanyika papo hapo bandarini na mara baada ya kumalizika, utasafirishwa kwa basi maalumu la kukodi kupelekwa Tanga.
Kaimu Mhariri Mtendaji wa UPL, Ramadhani Mkoma, amethibitisha mazishi ya marehemu Amina kufanyika Tanga.
Ramadhani amesema amepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa kwa sababu hakutarajia iwapo Amina angetangulia kuondoka duniani katika umri mdogo.
Amesema Amina ameacha pengo kubwa kwa sababu alikuwa mmoja wa wanahabari wa UPL waliokuwa wakifanyakazi kwa kujituma, aliipenda kazi yake na ilikuwa mwiko kwake kusukumwa kutimiza wajibu wake.
Amesema kazi aliyoifanya wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo alitumwa kuandika habari zake, ni uthibitisha wa wazi wa utendaji mzuri aliokuwa nao.
Amesema hawana la kufanya isipokuwa kumshukuru Mungu kwa kuwa kila alipangalo, hakuna anayeweza kulipangua. Amewataka wafanyakazi wa UPL kumuenzi Amina kwa kuiga utendaji wake wa kazi.

No comments:

Post a Comment