STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, December 29, 2013

Rage funika bovu...awagaragaraza akina Kinesi hivi hivi

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
MWENYEKITI wa Simba, Ismail Aden Rage amewagaragaza wapinzani wake baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kumtambua na kumtaka aitishe Mkutano Mkuu kwa klabu hiyo kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili imebaini upungufu kadhaa wa kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha Mwenyekiti wao.
Upungufu huo ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.
Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.
Hivyo, agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe mkutano lipo palepale. Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.
Katika mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.
TFF inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.
Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao vilivyofanya uamuzi wa kumvua madaraka Katibu wake Riziki Majalla.
Ajenda na muhtasari unaotakiwa ni wa vikao vya Kamati ya Utendaji iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi yake, na Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.
Aidha, TFF imewataka wanachama wake kuheshimu uamuzi halali unaofanywa na vyombo vyake kwa kuzingatia katiba na kanuni zake.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imetoa maelekezo hayo baada ya klabu ya Stand United kukata rufani kupinga uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuagiza mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Kanembwa JKT iliyovunjika kurudiwa Februari Mosi mwakani mjini Tabora.
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha suala hilo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ili itoe mwongozo kwa vile uamuzi huo uliofanywa na TPLB hauwezi kukatiwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za ligi husika.
Kamati imesisitiza kuwa hiyo ni falsafa ya mpira wa miguu ambapo uamuzi unaofanywa uwanjani haukatiwi rufani, hivyo uheshimiwe kama ilivyo kwa masuala ya mpira wa miguu kutopelekwa katika mahakama za kawaida za kisheria.
Wakati huo huo: Wanachama wa klabu ya Pan African wametakiwa kufuata ngazi husika pale wanapoona viongozi wa klabu yao wanakwenda kinyume na Katiba yao.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imetoa mwongozo huo kwa wanachama wa Pan African baada ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kulalamikia uongozi wao wakati wao si wanachama wa TFF.
Wanachama hao wanalalamikia uongozi wa klabu yao kwa kuitisha mkutano wa uchaguzi kabla ya ule wa kawaida ambao unatakiwa kufanyika mara moja kwa mwaka.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imelazimika kutoa mwongozo huo kwa vile wanachama hao katika malalamiko yao wamekigusa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) ambacho ni mwanachama wa TFF.
Pan African ni mwanachama wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala (IDFA) ambao ndiyo wanachama wa DRFA. Hivyo, TFF imemtaka mwanachama wake DRFA kupitia IDFA kufuatilia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment