STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 12, 2014

Wanawake, viongozi wa kitaifa, waalikwa Maulid Dar

MWENYEKITI Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Maulid kwa wanawake wa    mkoa wa Dar es Salaam, kuadhimishwa kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W),  Aisha Sururu (wa kwanza kulia), akiwaongoza wanawake wengine kuomba dua, baada ya kumaliza kikao cha maandalizi ya sherehe hizo
zitakazofanyika kesho, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
***
WANAWAKE viongozi wa kitaifa na mkoa wa Dar es salaam, wameombwa
kujitokeza ili kuungana na wanawake wengine wa kiislam, katika
sherehe ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W).

Wito huo ulitolewa na Kamati ya Maandalizi ya sherehe hizo kwa upande
wa wanawake, na kubainisha kuwa hawataalika mgeni rasmi, badala yake ,
viongozi na wanawake wengine wawe kitu kimoja kuadhimisha siku hiyo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aisha Sururu, alisema, sherehe itafanyika
Januari 14, katika ukumbi wa Diamond Jubilee, na kwamba
itawakutanisha wanawake waislam wa mkoa wa Dar es Salaam na mkoa
jirani wa Pwani.

"Wanawake wa hali ya chini, wamefikiria kwanini sherehe za kidini
ambazo hazina harambee, michango wala kitu chochote, tualike mgeni
rasmi? Wakaona ni vyema kutangaza ili nao kama wananchi wajumuike na
wanawake wa hali ya chini, ambao watafarijika zaidi, kuona wamekaa
mkekani pamoja na viongozi wakubwa,"alisema
Aisha.

Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni diwani viti maalum Ilala, alisema, kwa
wale ambao hawatafikiwa kwa mualiko wa mmoja mmoja, wanaruhusiwa
kujumuika na wenzao siku hiyo ya maadhimisho.

Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), huadhimishwa duniani  kote kila ifikapo mfungo wa sita kwa kalenda ya kiislam. ikiwa ni

kumbukumbu tangu kuzaliwa kwa kiongozi huyo wa wafuasi wa dini ya
kiislam.

Maandalizi ya sherehe hiyo kitaifa, mwaka huu yatafanyika mkoani
Kigoma, ambapo Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), limesema
mgeni rasmi atakuwa Rais Jakaya Kikwete.

No comments:

Post a Comment