STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 26, 2013

Jina la Rais Kikwete lahusishwa kutaka kupora ardhi ya wanakijiji Bagamoyo

Katibu wa wamiliki wa mashamba na makazi wa kijiji cha Buma, Gumbo Majibwa akisoma taarifa kwa wananakijiji wenzake, huku pembeni yake Mwenyekiti Hassani Tenela akimsikiliza kwa makini katika mkutano wao wa kupinga kutaka kuchukuliwa kwa maeneo yao ili kumpish mradi wa hospitali ya kimataifa inayodaiwa itamilikiwa JWTZ
Mmoja wa wamiliki wa mashamba na makazi wa kijiji cha Buma akiandikisha jina katika karatasi ya mahudhurio

Sehemu ya wahudhuriaji wakisikiliza kwa makini taarifa juu ya sakata la kutaka kuporwa kwa maeneo yao


Wamikili wa mashamba na makazi kijiji cha Buma, wilaya ya Bagamoyo wakiwa kwenye mkutano wao uliofanyika juzi Jumamiosi
Mpaka kieleweke hapa....Ardhi yetu anaitaka Rais au Jeshi? wanaulizana wamamiliki wa ardhi ya kijiji cha Buma

Najiorodhesha ili wasiseme sikuwepo!
Khadija Omary mmoja wa wanaomiliki ardhi katika kijiji cha Buma akitoa hoja na kuuliza maswali katika mkutano wao wa Jumamosi.

Viongozi wa Kamati waliosimama kando ya gari wakisoma taarifa kwa wamiliki wenzao kuhusu sakata la kutaka kuporwa kwa ardhi yao,.

Na sisi tumo mpaka kieleweke!

Hata iwe vipi ardhi yetu haiwezi kuchukuliwa kienyeji


Husna Mohammed naye hakuwa nyuma kutoa maoni yake. Mwanamama huyo ni mmoja wa watu sita walioteuliwa katika kamati maalum ya kwenda kumuona Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa ili kujua ardhi yao inachukuliwa na mwekezaji aliyetafutwa na Rais au ni JWTZ

"Tujiadharini isije kuna matapeli wanalitumia jeshi na jina la Rais kutaka kupora eneo leo. Hospitali gani inayojengwa katika eneo la ekari 1500? Dk Ally Ponza alihoji katika makutano huo
Tupo nanyi mwanzo mwisho mpaka kieleweke, hatukubali kirahisi kuachia ardhi yetu.

Frank Lyimo naye alitaka upatikane uthibitisho juu ya nani anayetaka kuchukua ardhi yao ili wasije wakambebesha lawama Rais Kikwete bure wakati kumbe hajui chochote kinachoendelea katika kijiji cha Buma.

Tupo pamoja

Katibu Gumbo Majubwa akitoa ufafanuzi baada ya kuulizwa na wanakijiji wenzake

Umoja ni nguvu! Hapa mwanzio mwisho mpaka tujue ukweli

Mwenyekiti wa kamati Hassan Tenela akifafanua jambo kwa wamiliki wenzake kuhusu ufuatuiliaji wao juu ya sakata la kutaka kuporwa ardhi yao.

"Jamani, tumeelezwa jeshi limetumwa tu kusaka ardhi, lakini mwekezaji ametafutwa na Rais alipokuwa nje ya nchi, lakini cha ajabu Mbunge wetu hajui na wala bajeti ya kulipwa fidia kwa kuporwa ardhi haipo kwenye Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ya 2013-2014' Mwenyekiti Hassan Tenela akiwafafanulia wenzake mahali alipofikia.
JINA la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete linadaiwa kutumika kuwatisha wamiliki wa mashamba na makazi wa Kijiji cha Buma, kilichopo Kata ya Kiromo wilaya ya Bagamoyo-Pwani ili waachie maeneo yao yanayodaiwa kutaka kuporwa kwa kisingizio cha kupisha mradi wa hospitali kubwa ya kimataifa inayodaiwa itamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wamiliki hao walitoa tuhuma hizo katika mkutano wa pamoja na  viongozi wa kamati yao, uliofanyika siku ya jumamosi kijiji hapo, ambapo uongozi wa kamati yao ulisema kuwa baada ya awali kuelezwa kwamba mradi huo ni wa JWTZ sasa wanaambiwa unahusu Rais Kikwete.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hassani Tenela alisema katika kufuatilia kinachoendelea juu ya mgogoro wa kuporwa maeneo yao, alielezwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chambezi, Abdallah Mchayungu kuwa, mradi huo siyo wa jeshi bali ni mradi uliopelekwa kwao na Rais Kikwete baada ya kupata mwekezaji nje ya nchi, hivyo ni lazima waachie eneo lao.
Hata hivyo alisema taarifa hiyo imewapa shaka na kuhisi kama jina la Rais linatumika ili kuwatisha kwa sababu awali walijulishwa ni jeshi linalotaka eneo lao ambapo bila kupata ridhaa yao waliweka alama (beacons) wakitaka eneo kwao na katika kijiji cha jirani cha Mataya.
"Kama mradi huo una mikono ya Rais, vipi mwenyewe kutowahi kuzungumzia kokote na kama ni jeshi mbona katika bajeti ya wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ya 2013-2014 hakuna fungu la fidia kwa vijiji vya Buma na Mataya? Katibu wa wamiliki hao, Gumbo Majubwa alihoji.
Majubwa alisema pia suala kwamba fidia ya kila ekari kutofautiana kati ya vijiji hivyo viwili inawapa shaka na kusema wanaendelea kushikilia msimamo wao wa kugoma kutoa maeneo yao hadi wahakikishwe mwekezaji halali anayetaka eneo hilo na wakae wakubaliane naye.
Katibu huyo alisema taarifa walizonazo ni kwamba kwa wenzao wa Mataya waliolazimishwa na kuridhia kuachia maeneo yao watalipwa kila ekari Sh Mil. 3, wao wa Buma wakidaiwa watalipwa  Sh Mil 7-10 kwa kila ekari kitu kinachomshangaza kwa vile ardhi inayochukuliwa ni moja.
Mara baada ya uongozi wa wamiliki hao kutoa taarifa hiyo, baadhi ya wamiliki walisema licha ya kwamba tangu awali walikuwa na shaka na mradi ulioelezwa utafanyika katika vijiji hivyo vya Buma na Mataya ukihusisha eneo la ekari 1500, kutajwa kwa Rais Kikwete linawatia shaka zaidi.
"Tunaomba uongozi wa kamati ufuatilie ukweli kama mradi huu unamhusisha Rais au jina lake linatumika kama njia ya kututisha, kwani pia zipo taarifa kwamba hata Mbunge wetu Dk Shukuru Kawambwa hajui lolote kuhusu mradi huu," alisema Dk Ally Ponza.
Dk Ponza, pia alisema kwa ufahamu wake ekari 1500 kwa mradi wa hospitali tu ni kubwa mno na kuhoji isije  ikawa ni matapeli wanaotaka kulitumia jeshi au jina la rais kuwapora ardhi yao ambayo wanamiliki kwa miaka mingi iliyopita.
Wamiliki wengine pamoja na uongozi wa kamati yao ulimtuhumu diwani wao, Hassan Usinga, wakidai wanahisi anawazunguka na kushiriki katika kutaka kuporwa kwa ardhi yao hasa kutokana na usaliti wanaodai amekuwa akiuonyesha tangu saka hilo lilipoanza.
"Katika mkutano tuliofanya Agosti 17 alitamka mwenyewe akidai yu tayari kumpa mwanakijiji wa Mataya viwanja vitatu vilivyopimwa na vyenye hati vilivyo barabarani ili atoe eneo lake kupisha mradi huu, tujiulize iweje awe tayari kutoa eneo lake kwa mradi usiomhusu?" Alihoji Samuel Lema.
Naye Husna Mohammed, alisema wanahisi viongozi wa kitongoji na kijiji chao pamoja na diwani lao moja na wanafanya mipango kuporwa ardhi yao kwa kuwalazimisha kama wenzao wa Mataya na kutaka kuugomea mkutano waliouitisha viongozi utakaofanyika Septemba 7.
Baada ya majadiliano marefu hatimaye wamiliki hao na uongozi wao uliazimia mambo matatu kuunda kamati ya watu sita kufuatilia ukweli wa mtu anayetaka kuchukua eneo lao kama ni Mwekezaji wa Rais Kikwete au jeshi, kuonana na Mbunge wao Dk Kawambwa ili awape ufafanuzi juu ya kuwepo kwa mradi huo au la.
Pia kuuzuia mahakamani mkutano ulioitishwa na uongozi wa kijiji utakaohudhuriwa na wanaodaiwa wawakilishi wa jeshi wanaoitaka ardhi yao, mpaka kwanza wapate uthibitisho wa kuwepo kwa mradi huo wa hospitali.
Katika kutaka kupata ufafanuzi wa sakata hilo na tuhuma zilizoelekezwa kwake, MICHARAZO lilimsaka Diwani Hassan 'Wembe' Usinga' kwa njia ya simu ambapo kwanza alikanusha suala la kuwasaliti wapiga kura wake akidai mradi huo ulipitishwa na wanakijiji wenyewe mwaka 2010.
Hata hivyo alikiri juu ya ahadi yake ya kumpa mwanakijiji wa Mataya aliyemtaja kwa jina la Mzee Nyanza viwanja vitatu ili atoe ardhi yao kama njia ya kumsaidia kutoka porini na kukaa barabarani na kudai  siyo kama kuna mkono wake katika mradi huo.
"Wamiliki hao wanashindwa kunielewa tu, mimi nipo hapa kusimamia haki zao ndiyo maana umeitishwa mkutano Septemba 7 ili wazungumze na wanaotaka ardhi yao, kudai mimi nawasaliti ni kutaka kunionea kwani mradi ulitambulishwa tangu 2010, wakati sijawa diwani," alisema diwani huyo.
Aliongeza kilichotokea ni kweli haya yeye hakuwa anaujua mradi huu na kuufuatilia na kugundua waliokuwepo wakati mradi ukipitishwa waliouza maeneo yao kwa watu wengine ambao ndiyo wanaoibua hoja za kuugomea, huku akikana mradi huo kumhusu Rais Kikwete na kusisitiza ni mradi wa Jeshi, ingawa alishindwa kufafanua iweje lichukuliwe eneo kubwa la ekari 1500 huku bajeti la kulipia fidia haikutajwa katika bajeti ya 2013-2014 ya wizara yao.
"Aaah wanataka eneo hilo, lakini walisema wataanza kulipa eneo la eka 250 au 300 kwa vile bajeti waliyonayo kwa sasa inahusu eneo hilo, japo mpaka sasa bado utathimini wa kiwango cha malipo hakijaanza na siyo kweli kama fidia zinatofautiana katika vijiji hivyo," alisema diwani huyo.
Alifafanua kuwa ni kweli wanajeshi hao waliweka alama bila kuwashirikisha wamiliki halali wa maeneo hayo, akidai walifanya hivyo kuweka alama ya eneo wanalolihitaji kwanza na sasa ndiyo wameanza tararibu za kutaka kulimiki kihalali eneo hilo na kutaka wanakijiji kuelewa.
"Huu mradi utakuwa mkubwa kwa mujibu wa wawakilishi wa Jeshi waliokuja kujitambulisha kwa uongozi wa kijiji cha Buma Agosti 20, hivyo wananchi waupokee kwa moyo mmoja kwani una manufaa kwao, ingawa wana hiari ya kutoa eneo lao baada ya kujiridhisha," alisema.
Hata hivyo Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa ambaye ni Waziri wa Elimu na Ufundi, alipoulizwa mradi huo, alisema ofisi yake haina taarifa rasmi ya kina na kudai ataanza kuufuatilia ili ajue ukweli wa mradi huo kisha atatoa taarifa kwa vyombo vya habari.
"Ofisi yangu ina taarifa za juu juu tu, tumeanza kufuatilia kujua ukweli ila nitahadharishe wananchi wawe makini na miradi inayoibuliwa hivi sasa ili wasiingwe mkenge," alisema Dk Kawambwa.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Ahmed Kipozi alipotafutwa na MICHARAZO alisema asingekuwa tayari kuzungumza suala hilo kwa vile suala hilo lipo chini ya Afisa Ardhi, ingawa alisema wilaya yake suala la migogoro ya ardhi imekuwa kama fasheni na kuikuta tangu aingie madarakani.
"Kwa kweli siwezi kufafanua lolote kuhusu suala la kijiji hicho cha Buma au kwingineko kwa sababu wanaohusika kutoa majibu kamili ni afya ardhi, ila ukweli migogoro ya ardhi hapa Bagamoyo ni ya kawaida, ni vyema kama ukija kupata ufafanuzi zaidi," alisema DC huyo.

No comments:

Post a Comment