STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, March 4, 2013

Ndomba: Mkali wa ngumi anayeota makubwa kimataifa

Bondia Pascal Ndomba



Bondia Pascal Ndomba akiwa Marekani
WAKATI mabondia wengi nchini, wakiwamo wenye majina makubwa, wakilia juu ya mchezo wa ngumi kutowapa mafanikio ya kujivunia, kwa Pascal Ndomba hali kwake ni tofauti.
Bondia huyo anayefahamika zaidi kama 'Kimondo', anasema ngumi zimempa mafanikio ya kujivunia kiasi kwamba hajutii kuucheza mchezo huo.
Ndomba anasema mbali na ngumi kumwezesha kuzitembelea nchi mbalimbali duniani, lakini pia zimemfanya ajenge nyumba Kimara Suka, akimiliki kiwanja eneo la Mbezi Beach pamoja na kuitunza vema familia yake.
Bingwa huyo wa zamani wa Taifa wa TPBC na Afrika Mashariki na Kati, anasema na hivi karibuni ameingia mkataba nchini Marekani ambao unamfanya azidi kuuheshimu mchezo huo.
Anasema mkataba huo wa muda wa miaka minne aliingia mwishoni mwa mwaka jana na kampuni ya Nelson Boxing Promotion na umeanza kutumika mwaka 2013 hadi 2017.
"Ingawa ni kweli ngumi kwa hapa nchini na hata kanda ya Afrika Mashariki zimekuwa hazina tija kutokana na ubabaishaji uliopo, nashukuru Mungu zimenisaidia kwa mengi," anasema.
Anasema siri ya kufanikiwa kupitia mchezo huo ni kujitambua kwake na kuwa na nidhamu kwa kila senti anayoipata, huku akimwagia sifa 'bosi' wake Humoud M. Sumry, anayemfadhili.
"Bosi wangu Humoud Sumry, ndiye kila kitu kwangu kwa msaada anaonipa chini ya kampuni yake ya mabasi ya Sumry," anasema.


SIRI
Bondia huyo anafichua siri kwa kusema kuwa chanzo cha mabondia wengi nchini na hata Afrika kushindwa kufanikiwa kimaisha na kimichezo kupitia ngumi inatokana na ubabaishaji uliopo katika sekta hiyo.
Anasema mapromota na viongozi wa ngumi wamekuwa wakiwanyonya mabondia kwa kutumia udhaifu wao wa kuwa na elimu ndogo ama kushindwa kujitambua wapo katika mchezo huo kwa ajili ya nini.
Pia anasema kumekuwa na hila zikifanywa kati ya viongozi wa vyama na mapromota wa nje wa kutaka mabondia dhaifu ndiyo wapelekwe nje kuicheza na hata kama ni wakali basi hulazimishwa wacheze chini ya kiwango.

Pascal Ndomba akiwa nje ya nchi
"Hufanya hivyo kwa lengo la kutaka mabondia wao kuendeleza rekodi zao na ikitokea bondia anayepelekwa huko akashinda kama alivyofanya Karama Nyilawila basi huzua tafrani baina ya pande mbili zilizokubaliana," anasema.
Akaongeza hiyo ndiyo sababu inayofanya mabondia wengi wa Tanzania au barani Afrika kupigwa kila wanapoenda nje.
"Ni 'dili' tu zinazofanywa na baadhi ya watu wachache kwa tamaa za fedha," anasema.
Ndomba anayependa kula ugali au ndizi kwa nyama na kunywa Fanta, pia anasema mabondia wamekuwa wakidhulumiwa haki zao na baadhi ya viongozi wa ngumi kwa kuwapunja fedha za malipo tofauti na makubaliano.

Pascal Ndomba akiwa na 'bosi' wake, Humoud Salim
Anasema inawezekana bondia ameitwa kwenda kucheza nje kwa dola 5,000, lakini huishia kulipwa 3,000 au nusu ya hapo kwa kisingizio hiki na kile, wakati mwingine asipewe kabisa.
Bondia huyo aliyeingia kwenye ngumi kwa kuvutiwa na bingwa wa zamani wa dunia, Mike 'Iron' Tyson, anasema ni vema kungekuwa na utaratibu chini ya serikali kuhakiki mikataba na kujua kinachompeleka bondia nje ya nchi.
"Japo hizi ni ngumi za kulipwa, ni vyema kungekuwa na chombo cha namna hiyo kusimamia safari za mabondia nje kuepusha kudhulumiwa na kuichafua nchi nje kwa vile hupeperusha bendera ya taifa," anasema.

MATAJI
Ndomba, mume wa Ikupa aliyezaa naye watoto wawili, Michael (8) na Abel (5) wanaosoma Shule ya Msingi Makuburi, anasema alianza rasmi ngumi mwaka 1996 katika klabu ya Kiwira iliyopo Kyela Mbeya.
Kocha aliyemnoa anaitwa Said Tambwe na alishiriki michuano kadhaa ya ngumi za ridhaa na alipoona hazina tija yoyote, mwaka 2000 aliamua kuhamia ngumi za kulipwa.
Anasema akizcheza ngumi hizo aliweza kunyakua ubingwa wa mkoa wa Mbeya na kupata fursa ya kupigania ubingwa wa Taifa wa TPBC mwaka 2005 kwa kumpiga Fike Wilson.
Aliendelea kutoa vipondo kwa wapinzani wake kabla ya mwaka 2009 kutwaa taji la Afrika Mashariki na Kati kwa kumchapa kwa KO Mkenya Joseph Odhiambo.
Pia amewahi kuwania mikanda ya kimataifa inayotambuliwa na WBC, WBO na IBF, uzito wa Cruiser mara ya mwisho ikiwa Desemba, 2012 alipoenda Ghana kupigana na Mghana asiyepigika Braimah Kamoko na kunyukwa.

Pascal Ndomba (Kushoto) akichapana na Mghana Braimah Bamoko
Ndoto zake kubwa ni kuja kutwaa ubingwa wa dunia akiamini ana uwezo wa kufanya hivyo, pia akitamani kuja kumiliki gym na klabu ya kufunzia vijana mchezo huo.
"Napenda nije kuwafunza na kuwarithisha vijana kipaji changu, najua siwezi kusalia kuwa bondia milele," anasema.
Licha ya kucheza mapambano mengi, Ndomba analitaja pambano la kuwania ubingwa wa vijana wa IBF uzani wa 'cruiser' dhidi ya Mswisi, Agron Dzila, kuwa ndilo gumu kwake na asiloweza kusahau kwa 'kisago' alichoikipata.

CHIMBUKO
Pascal Ndomba alizaliwa mwaka 1983, Kyela Mbeya akiwa ni mtoto wa nne kati ya watano wa familia yao na alisoam  Shule ya Msingi Lema ya Kyela kabla ya kujiunga Tabora Boys kwa masomo ya Sekondari.
Tangu shuleni alipenda michezo, ila alivutiwa na ngumi na kujifunza kabla ya kuanza kuzipiga ulingoni na mabondia kama akina Bagaza Mwambene, George Sabuni, Hassani Matumla, Karama Nyilawila na Maneno Osward.
Ndomba anasema hana furaha mpaka atakapopanda ulingoni kupigana na Japhet Kaseba aliyenukuliwa hivi karibuni akidai amekuwa akikwepa na baadhi ya mabodnia kwa umahiri wake.
"Kwa kweli kiu yangu ni kuzichapa na Kaseba, dai lake kwamba amekuwa akikimbiwa na mabondia siyo kweli kwa vile nimekuwa nikiomba kucheza naye bila mafanikio," anasema.
Ndomba anayeiomba serikali itupie macho mchezo wa ngumi kwa madai umekuwa ukiiletea sifa Tanzania nje ya nchi kwa mabondia waliowahi kutwaa mataji ya kimataifa.

Pascal Ndomba (kushoto) akiwa kwenye kazi yake ya uwakala wa mabasi kituo cha mabasi cha Ubungo
Bondia huyo anayependa kusikiliza muziki na kuangalia runinga mbali na kucheza ngumi pia ni wakala wa kampuni ya mabasi ya Sumry, akiishabikia Simba na Manchester United, na anawazimia Shomari Kapombe na Patrick Evra.
Tukio la furaha kwa Ndomba, ambaye anamkubali sana bondia mkongwe Mbwana Matumla, ni siku mkewe alipojifungua mtoto wake wa kwanza mwaka 2005. "Tukio la huzuni nisilolisahau ni kifo cha baba yangu kilichotokea mwaka 2002," anasema.

Pascal Ndoma (kushoto) akiwa na wakala mwenzake wa mabasi ya Sumry

No comments:

Post a Comment