STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 18, 2015

Wenyeji AFCON waanza na sare, Gabon yaua 2-0

Nahodha wa Guinea ya Ikweta, Emilio Nsue akiifungia timu yake bao katika mechi dhidi ya Kongo
Pierre-Emerick  Aubameyang akishangilia bao la kuongoza na Gabon wakati akiiongoza timu yake kushinda mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso (Picha:SuperSport)
Mashabiki wa soka nchini Guinea ya Ikweta wakimimika uwanjani kushuhudia ufunguzi wa michuano hiyo mjini Bata
BATA, Guinea ya Ikweta
FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zimeanza kwa kishindo kwa kushuhudiwa wenyeji, Guinea ya Ikweta ikilazimishwa sare ya 1-1 huku Gabon wakiifumua wanafainali zilizopita, Burkina Faso kwa mabao 2-0 katika mechi za ufunguzi zilizochezwa mjini Bata.
Wenyeji wakiwaanikizwa na washangiliaji wao, walitangulia kupata bao katika mechi ya mapema kupitia kwa Nsue aliyefunga katika dakika ya 16 kabla ya Kongo kuchomoa zikiwa zimesalia dakika tatu kupitia kwa Thievy Bifouma na kuwanusuru wakali kuambulia pointi moja katika kundi lao la A.
Katika mechi iliyofuata, Gabon ikiongoza na mshambuliaji nyota anayeichezea Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang wakipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso.
Aubameyang alianza kwa kufunga bao la kuomngoza katika dakika ya 19 kabla ya Malick Evouna kuongeza bao la pili lililowakatisha tamaa 'Farasi Weupe' wa Burkinabe baada ya kufunga bao katika dakika ya 72.
Katika mfululizo wa michuano hiyo leo timu za Kundi B zitashika dimba la Ebebiyin kwa  mabingwa mara tatu wa fainali hizo, Tunisia watavaana na Cape Verde huku  Zambia wakitarajiwa kuumana na DR Congo.
Zambia na DR Congo ndiyo watakaoanza kuumizana saa 1 usiku kabla ya Tunisia na Cape Verde kukutana katika mechi ya kisasi baada ya timu hizo kufanyiana mtimanyongo kwenye mechi za kuwania fainali za Kombe la Dunia kwa Tunisia kuichongea Cape Verde waliokuwa wamefuzu hatua ya mwisho kwa madai ya kumtumia mchezaji asiyestahili na Cape Verde kuzikosa fainali hizo, ingawa Tunisia walikwama licha ya kupeta katika rufaa yao baada ya kung'oka kwa Algeria walioenda kufanya maajabu kwa kufika raundi ya 16 Bora.
Jumla ya timu za mataifa 16 zinachuana kwenye fainali hizo ambazo zinachezwa Guinea ya Ikweta baada ya Morocco kugoma kuiandaa kwa madai ya kuhofia maambukizo ya Ugonjwa wa Ebola.
Kitu cha kustaajabisha ni kwamba waliokuwa mabingwa watetezi NIgeria wameshindwa kwenda kwenye fainali hizo zinazochezwa kuanzia jana na kutarajiwa kumalizika Februari 8 ambapo bingwa mpya atafahamika.

No comments:

Post a Comment