STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 21, 2013

SIMBA, YANGA NANI MTANI JEMBE TAIFA LEO?

Yanga


Simba

KUANZIA Mitaani, vijiweni mpaka maofisini na kwenye daladala gumzo na tambo ni pambano litakalochezwa jioni ya leo kati ya Simba na Yanga.
Nguo na bendera zenye rangi zinazovaliwa na klabu za timu hizo ndizo zilizotapakaa mitaani huku kila mtu akisema leo ndiyo leo, akitambia timu yake.
Hata hivyo ukweli na jibu kamili la nani mbabe au Nani Mtani Jembe kama pambano hilo la kirafiki maalum lilivypewa jina litafahamika baada ya dakika 90.
Klabu hizo mbili wapinzani wa jadi wa soka nchini zitashuka dimba la uwanja wa Taifa kuumana ikiwa ni miezi miwili tu tangu zilipotoshana nguvu kwa kutoka sare ya mabao 3-3 kwenye uwanja huo huo.
Tofauti na mechi ya leo, katika mechi yao iliyochezwa Oktoba 20, Simba na Yanga zilizokuwa zikipimana ubavu kwenye pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga walitangulia kupata mabao matatu yaliyofungw ana Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza 'Diego' kabla ya Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kazze kurejesha mabao hayo kipindi cha pili.
Hivyo mashabiki na wanachama wa timu hizo kila mmoja pamoja na kutamba mtaani, lakini presha zao zitakuwa juu kabla na baada ya dakika 90 za pambano hilo kutokana na aina na vikosi vyao.
Yanga ikiwa na kocha yule yule, Ernie Brandts itaikabili Simba ikiwa na silaha mpya tatu, kipa Juma Kaseja, kiungo Hassan Dilunga na mshambuliaji Emmanuel Okwi aliyekuwa gumzo kwa wiki nzima juu nchini.
Ujio wa Okwi umekuwa gumzo na kufunika kila kitu katika soka la Tanzania kutokana na ukweli ni kati ya wachezaji waliokuwa wakiinyima Raha wakati akiichezea Simba.
Ndiye aliyekuwa mwiba mkali wakati Yanga ikilowa mabao 5-0 toka kwa Mnyama akifunga mawili na kusaidia mengine yaliyowafanya Jangwani wawe na deni jingine kubwa toka kwa watani zao.
Deni hilo ni mbali na lile waliloshindwa kulilipa kwa zaidi ya miaka 30 waliponyolewa 6-0 mwaka 1977.
Hata hivyo Simba ikiwa imebadilisha benchi la ufundi kwa aliyekuwa kocha mkuu, Kibadeni Abdallah King na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelu 'Julio' kutimuliwa Msimbazi na nafasi zao kuchukuliwa na Mcroatia.
Mbali na kocha huyo, pia Simba ina wachezaji kadhaa wapya akiwamo makipa Ivo Mapunda na Yew Berko waliowahi kuichezea Yanga, beki toka Kenya, Donaldo Musoti na viungo, Badru Ally na Awadh Juma na huku Uhuru Suleimana akirejea kikosini toka Coastal Union.
Tusubiri tuone nani atakayemtambia mwenzake baada ya dakika hizo 90 au mikwaju ya penati kama watashindwa kuonyeshana ubabe, lakini TFF kupitia Kaimu Katibu Mkuu na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema maandalizi ya mechi hiyo ya aina yake yamekamilika.
Wambura alisema vikosi vya ulinzi na usalama katika mechi ya leo vimekamilika kila idara na kwamba Barabara ya Taifa inayoanzia Keko-Maghorofani hadi Barabara ya Mandela, itafungwa kuanzia saa 12 asubuhi kupisha hekaheka za mtifuano huo.
Alisema magari hayataruhusiwa kuegeshwa kuanzia eneo la Baa ya Minazini hadi msikiti unaotazamana na Uwanja wa Uhuru, hivyo magari yote yataegeshwa nje ya Uwanja wa Ndani wa Taifa – kando ya Barabara ya Mandela.
“Magari yatakayoruhusiwa kuingia maeneo hayo na hata ndani ya Uwanja wa Taifa ni yatakayokuwa na stika zilizotolewa na TFF. Tunawaomba wadau na mashabiki wa soka kuheshimu na kutii maagizo ya vikosi vya ulinzi,” alisema Wambura.
Aliongeza kuwa milango ya kuingilia uwanjani itakuwa wazi kuanzia saa sita mchana ambapo baada ya mauzo ya tiketi ya jana, zoezi hilo litaendelea leo nje ya uwanja huo kabla ya mechi ili kuwapa mashabiki fursa ya kukata na kuingia moja kwa moja.
Viingilio vya leo  cha chini ni sh 5,000 kwa viti vya kijani, huku upande wa viti vya rangi ya bluu, kiingilio ni sh 7,000; viti vya rangi ya chungwa sh 10,000; VIP C ni sh 15,000; VIP B sh 20,000 huku VIP A sh 40,000.
Kwa upande wa waamuzi, kati atasimama Ramadhan Ibada ‘Kibo’ wa Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba na Simon Charles wa Dodoma huku Israel Nkongo wa Dar es Salaam akiwa mezani. Kazi ya kutathimini utendaji wa waamuzi wote itakuwa chini ya Soud Abdi wa Arusha.

MECHI TANGU 2010
Rekodi ya watani hawa inaonyesha kuwa mechi ya leo ni ya tisa tangu 2010 na katika mechi nane, Yanga imeshinda tatu, Simba mbili na wamekwenda sare tatu.
Aprili 18, 2010: Simba 4, Yanga 3
Oktoba 16, 2010: Yanga 1, Simba 0
Machi 5, 2011: Yanga 1, Simba 1
Oktoba 29, 2011: Yanga 1, Simba 0
Mei 6, 2012:  Simba 5, Yanga 0
Oktoba 3, 2012: Yanga 1, Simba 1
Mei 18, 2013: Yanga 2, Simba 0
Oktoba 20, 2013: Simba 3, Yanga 3

No comments:

Post a Comment