STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 19, 2012

Paparazi asimulia magumu aliyopata akipiga picha mauaji ya Mwangosi

Mfumo wa picha uliotengenezwa na kurushwa na mitandao ya kijamii ukionyesha namna marehemu Daud Mwangosi aliyekuwa mwanadishi wa kituo cha Channel Ten alivyopoteza uhai wake hivi karibuni.
MPIGAPICHA mkongwe nchini wa gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga, ni kati ya walioshuhudia tukio la kuzingirwa, kuteswa hadi kuuawa kinyama na askari wa Jeshi la Polisi kwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi hapo Septemba 2, katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.
Senga, kati ya wapiga picha maarufu na wakongwe nchini waliopita katika magazeti mbalimbali, anayefanya kazi hiyo kwa takribani miaka 28 sasa, anasimulia aliyoyashuhudia siku hiyo wakati akitimiza wajibu wake.
Kubwa zaidi, Senga anasema ameweza kupata picha nyingi za ukatili huo uliofanywa na askari polisi dhidi ya Mwangosi, kuanzia kukamatwa kwake, kupigwa na kuteswa kabla ya kuelekezewa bunduki ya mdomo mpana katika tumbo na kuukatisha uhai wake.
Katika mahojiano maalumu, Senga anasema tangu kutokee mauaji yale ya kinyama ambayo yangeweza kumtisha yeyote yule kutokana na kufanywa na askari polisi wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao, mengi yamezungumzwa.
Anasema kinachomsikitisha zaidi, ni kitendo cha baadhi ya waandishi kuibuka na kudai kuwa sio tu walikuwepo karibu ya tukio hilo, pia ndio waliopiga picha zikionesha mauaji hayo ikiwemo ile ya askari aliyeelekeza mtutu tumboni kwa Mwangosi.
Senga anasema kwake haoni fahari yoyote kujitwika jukumu hilo la kuueleza umma kuwa alikuwa hatua chache tu wakati Mwangosi anafanyiwa unyama ule na askari polisi, bali ameamua kuweka sawa ili kuepuka upotoshwaji wa tukio hilo la kikatili lililogharimu uhai wa Mwangosi.
Anasema ameamua kufanya hivyo baada ya kubaini kuwa kupitia tukio hilo lililogusa wengi, baadhi ya watu ambao hawakuwepo kwenye eneo alilosulubiwa Mwangosi hadi kuuawa, wamejitwisha ushuhuda wa tukio hilo na kusema ni hatari kuleta maigizo kwenye tukio nyeti kama hilo.
Senga anasisitiza kuwa amekuwa kimya kuhusu jambo hilo, lakini baada ya kushauriwa na watu wenye busara wakiwamo wakuu wake wa kazi, akaona aeleze kilichotokea kuweka mambo sawa, japo hakutaka kwani hakuona ni tukio la kujipatia sifa isipokuwa simanzi isiyofutika haraka machoni.
Anasema licha ya kuifanya kazi hiyo kwa miaka yote hiyo na kuwahi kukumbana na kadhia nyingi, lakini mazingira ya kuuawa kwa Mwangosi, hatayasahau kamwe katika maisha yake yote atakayojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
“Jamani tukio la kuuawa kwa Mwangosi linatisha. Wakati anaburutwa, kupigwa, kuteswa na kundi la askari, usingeweza kusema ni mwandishi wa habari, pengine ungeweza kusema ni kibaka au jambazi, hakuwa na muda wa kujihami zaidi ya kusema ‘mnaniua mimi ni mwandishi’,” anasema Senga.
Anasema alishangazwa namna askari polisi walivyokuwa wamempania Mwangosi kwani alikumbana na mateso hayo akiwa na kamera mkononi na mkoba mdogo begani kwake, kuashiria hakuna kilichompeleka Nyololo, isipokuwa kutimiza wajibu wake.
Senga anasema cha kushangaza zaidi ni kuona askari wale walivyokuwa wamejawa na jazba iliyowafanya wampuuze hata bosi wao (aliyemkumbatia Mwangosi), ambaye licha ya kuwaeleza wamwache, wasiendelee kumtesa kwani anamjua, wakazidi kumshambulia wakati huo Mwangosi akijitetea na kuwasihi wamwache bila mafanikio.
Katika mazingira hayo, Mwangosi akiwa amezingirwa na askari kama nane hivi akiwemo mtetezi wa mwandishi huyo, na askari ambaye alikuja kujulikana jina lake baadaye kuwa ni Pacificus Cleophace Simon (G2372), akiwa karibu mno akaelekeza mdomo wa bunduki tumboni mwa mwandishi huyo na kumlipua.
Mbali ya kuusambaratisha mwili wa Mwangosi, alimjeruhi pia eneo la mapaja askari yule aliyekuwa akimtetea Mwangosi (OCS Mwampamba).
Kinachosikitisha zaidi, ni kwamba wakati wote huo askari wakimtesa Mwangosi, Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Iringa, Michael Kamuhanda, alikuwepo mita chache tu kutoka kwenye tukio, akiwa kwenye gari yake (angalia picha namba 7).
Kabla ya Mwangosi kupigwa bomu, mwandishi wa Tanzania Daima, Abdallah Hamis alimfuata Kamuhanda aliyekuwa ndani ya gari yake iliyofungwa vioo (pengine kuogopa moshi wa mabomu) na kuhoji vipi askari wanamsulubu Mwangosi?
Alichofanya Kamuhanda, ni kumpuuza Abdallah na alipoona anazidi kusumbuliwa, akashusha kioo kumsikiliza, lakini hakujibu kitu zaidi ya kufunga kioo na kutoa picha kuwa, alichokuwa akifanyiwa Mwangosi ni agizo lake au ni malipo aliyostahili kwa siku ile.
Senga anasema kwa kulishuhudia kwa macho yake tukio hilo la kinyama lililokatisha uhai wa Mwangosi, kamwe hataweza kulisahau kutokana na kufanywa katika mazingira ya kutisha na kuogofya huku yeye akipiga picha za kuteswa hadi kuuawa kwa bomu kikatili.
Mwanahabari huyo mkongwe amebainisha kuwa, katika tukio hilo aliweza kupiga picha karibia zote zilizotumika kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje, yakiwemo magazeti na hata televisheni, kubwa zaidi zikipingana na hila za Jeshi la Polisi kutaka kupindisha ukweli wa mambo.
Ikumbukwe, jioni ya siku ya tukio, Kamanda Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, bila hata hofu ya Mungu ndani yake, akaanza kudai eti kabla ya kutokea mlipuko wa bomu, Mwangosi alitokea upande wa wafuasi wa CHADEMA. Ni aibu na hatari kubwa kwa taifa.
Mazingira kabla ya kifo
Senga anasema asubuhi ya siku ya tukio, waandishi wa habari walialikwa katika mkutano na Kamanda Kamuhanda ambao ulifanyika ofisini kwake, mjini Iringa, yeye akiwa mmoja wao.
Anasema ulikuwa ni mkutano wa kutoa tamko la kuzuia mikutano ya kisiasa, lakini hususan iliyokuwa imepangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kilikuwa kinaendelea na mikutano yake mkoani humo baada ya kutoka Morogoro.
Polisi walitaka kusitishwa kwa mikutano hiyo kutokana na kile kilichoelezwa kuongezwa kwa muda wa zoezi la sensa kwa siku saba zaidi, baada ya zile siku saba za kwanza kumalizika huku lengo lililokuwa limekusudiwa kutotimia.
Senga anasema baada ya mkutano huo, waandishi walitaka kujua upande wa pili yaani CHADEMA, hivyo walielekea walikokuwa ambako nako kulifanyika mkutano na waandishi wa habari ukiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Baada ya zuio la mkutano
Senga anasema CHADEMA walitoa tamko wakilaumu utendaji wa Jeshi la Polisi kwa madai kuwa, lilikuwa likifanya kazi zake kwa kuongozwa na matakwa ya wanasiasa hususan wa chama tawala (CCM), lakini walisitisha mikutano yao japo kwa shingo upande.
“Katika mkutano wa waandishi wa habari na Kamanda Kamuhanda, yalijitokeza maswali mengi likiwemo la mikutano ya ndani iliyokuwa ikifanywa na CHADEMA, wakati wa zoezi la sensa likiendelea kabla ya kuongezwa zile siku saba, ambalo lilijibiwa na kamanda huyo, kwamba mikutano hiyo inaruhusiwa,” anasema Senga na kuongeza:
“Uongozi wa CHADEMA uliamua kuendelea na mikutano ya ndani ikiwa ni pamoja na kufungua matawi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa katika kila jimbo, wakati wakisuburi kumalizika kwa sensa ya awamu ya pili.”
Ufunguzi wa matawi
Senga anasema baada ya hapo ndipo Chadena wakajipanga kwenda kufanya zoezi hilo mchana wa siku hiyo kufungua matawi katika kijiji cha Nyololo kwa kuteua viongozi wawili kuongoza zoezi hilo bila kumshirikisha Katibu Mkuu, Dk. Slaa.
“Nakumbuka walipangwa viongozi wa kuendesha zoezi hilo akiwemo Naibu Katibu (Zanzibar), Hamad Yusuf na Kamanda wa Operesheni hiyo, Benson Kigaira. Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa hakushiriki kabisa siku hiyo, alibaki hotelini,” anaongeza Senga.
Mwangosi anasita kwenda katika ufunguzi
Wakati wa maandalizi ya kwenda katika ufunguzi wa matawi, Senga anasema Mwangosi alimwambia asingekwenda katika hafla hiyo kwa kuwa hakuona tena kama kungekuwa na habari kwani ilikuwa ni mikutano ya ndani tu.
Anasema kama ilivyo kawaida kwa wanahabari, kunusa na kutafuta habari zilipo, zilizagaa taarifa kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walikuwa wamemwagwa katika eneo ambalo CHADEMA wangefungua matawi katika kijiji hicho.
Kwa taarifa hizo, wanahabari wengi wakatamani kwenda kushuhudia ufunguaji huo wa matawi (akiwemo Mwangosi), pasipo kujua kuwa kumbe yeye ndiye anakwenda kuwa habari iliyotikisa nchi.
“Ni kweli ndivyo ilivyokuwa, baada ya kufika katika Kijiji cha Nyololo, tulikuta maandalizi yamekamilika, askari hao wakiwa na silaha za kila aina. Nilijua ni kazi yao pengine walipewa maelekezo ya kuwalinda viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA wakati wakifungua matawi yao ili kuwahakikishia usalama wao,” anasema Senga.
Hata hivyo, anasema fikra zake hizo zilianza kupotea baada ya kuanza kutolewa amri na viongozi wa Jeshi la Polisi wa mkoa huo, wakiongozwa na RPC Kamuhanda na RCO ambao kwa nyakati tofauti walionekana kutofautiana, mwingine akikubali kufanyika kwa zoezi hilo kwa vile halikuwa na madhara na mwingine akitaka kusitishwa.
Kwa mujibu wa Senga, CHADEMA walifanikiwa kufungua tawi la kwanza wakiwa wamezingirwa na askari, lakini hali ilibadilika wakati wakifungua tawi la pili ambako polisi walianzisha mapambano dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho.
“Nasema leo hatutapiga mabomu, tutakamata viongozi, wakamateni viongozi wote wa CHADEMA,” anasimulia Senga alivyosikia amri kutoka kinywani mwa RPC alipokuwa akiwaamuru askari wake kutekeleza amri hiyo.
Senga anasema kabla amri hiyo haijatekelezwa, ghafla yakaanza kulipuliwa mabomu ya machozi kutoka kwa askari polisi kwa lengo la kuwatawanya wana-CHADEMA waliokuwa nje ya ofisi hizo.
Wakati mgumu kwa wanahabari
Anasema viongozi hao walitawanyika huku hata wasio viongozi wakakimbia kusikojulikana. Hapo ndipo wakati mgumu ulipoanzia kwa wanahabari, kwa kubwia moshi mzito wa mabomu yaliyolipuliwa katika kila kona ya eneo hilo.
Kama vile hapakuwa na tukio la kulipuliwa kwa mabomu, Senga anasema baadaye utulivu ulirejea, lakini wakati huo hakukuwa na mwananchi hata mmoja akipita katika maeneo hayo, isipokuwa askari tu na baadhi ya waandishi wa habari.
Senga anasema aliendelea kutekeleza majukumu yake akiamini kuwa kwake mbele ya askari wale ni hakikisho la usalama ingawa baadhi yao walishaanza kuondoka baada ya kukamilisha kazi yao, wakitembea na mbele yao kukiwa na magari matatu yakielekea barabara kuu ya Dar es Salaam - Mbeya.
Mwangosi anaanza kusulubiwa
Anasema wakiwa katika msafara huo, ghafla aliona mtu akishambuliwa kwa kipigo na askari hao waliokuwa mbele yake, akashtuka na kujiuliza ni nani na kwa sababu gani kwani hali ya mambo tayari ilikuwa tulivu.
“Mmoja wa askari hao aliingilia kati na kumkumbatia, akiwazuia askari wenzake wasiendele kumpiga akisema: “mwacheni namfahamu ni mwandishi, acheni jamani,” akijaribu kuokoa uhai wa mtu huyo ambaye wakati huo miguu yake ilikuwa katikati ya miguu ya askari yule msamaria. Wakati huo akionekana kuishiwa nguvu kwa kipigo kikali,” anasema Senga.
Anasema licha ya jitihada kubwa za askari yule msamaria mwenye nyota tatu mabegani mwake kuwazuia wenzake wasiendelee kumpiga, bado kundi la askari wale waliendelea kumpa kipigo. Baadaye alimtambua kwa ukaribu kuwa alikuwa ni Daudi Mwangosi.
Wakati hayo yakiendelea, Senga anaeleza kuwa, akili yake ilimkumbusha kuwa alikuwa kazini, hivyo pamoja na huruma ya kuguswa na unyama ule, pia akapaswa kuchukua picha za tukio hilo bila kujali kitu gani kingempata kutoka kwa askari wale wenye hasira iliyopitiliza.
Anaongeza kuwa, ghafla mmoja wa askari hao alimkaribia na kumshika mkono kabla ya wengine wawili kuongezeka, wakamzonga sana, wakati huo Mwangosi akiendelea kusulubiwa.
“Tukupeleke pale na wewe?” lilikuwa swali kutoka kwa askari hao kwa Senga, akimaanisha pale alipokuwa akisulubiwa Mwangosi. Senga anasema wakati huo hakuwa na jibu la haraka.
Mwangosi alipuliwa
Senga anasema wakati askari hao wakiwa bado wanamsulubu Mwangosi, ghalfa akasikia mlipuko mkubwa na kwa macho yake, akashuhudia wale askari waliokuwa wamemzingira wakatawanyika kwa taharuki.
Anasema baadhi yao walionekana wakielekea kwenye magari yaliyokuwa mbele, wakati huo Kamanda Kamuhanda akiwa umbali kama wa mita tano hivi ndani ya gari yake iliyokuwa imefungwa vioo vyote.
Senga anasema baada ya mlipuko ule alichoweza kushuhudia ni nyama zilizosambaa huku kando yake akiwepo askari (yule aliyekuwa akimtetea kabla ya kulipuliwa kwake), akiwa amejiinamia kando ya mabaki hayo ya mwili wa Mwangosi, naye akiwa amejeruhiwa sehemu ya paja la kushoto.
Anasema tukio hilo lilimfanya abaki ameduwaa kwa dakika chache asijue la kufanya, kwani ni mara yake ya kwanza kuona unyama na ukatili wa kiwango hicho, tena ukifanywa na askari polisi kwa mtu asiye na silaha yoyote zaidi ya begi na kamera mkononi mwake.
“Swali kubwa ambalo nilijiuliza moyoni mwangu, ni kama kweli nilichokuwa nikishuhudia mbele yangu ulikuwa mwili wa Mwangosi,” anasema Senga.
Katikati ya swali hilo, Senga anasema akakumbuka kuwa yu kazini, hivyo akaendelea kupiga picha za mabaki ya mwili wa Mwangosi, wakati huo kando yake akiwepo yule askari aliyekuwa akilia kwa uchungu akisema, “Afande wameniua.” Pengine akimweleza Kamuhanda aliyekuwepo karibu.
Anasema baadaye Kamuhanda akiwa ndani ya gari lake karibu na eneo la tukio, aliwaamuru askari warudi kumchukua askari yule majeruhi, hivyo wakarejea na kumbeba wakimweka kwenye gari.
Senga anasema dakika hizo chache kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwake, akibaki eneo hilo ameduwaa, akiangaza macho mbele na nyuma kwani wakati huo hakuona raia wa kawaida zaidi ya askari.
Anasema katikati ya butwaa hiyo, ufahamu ukaanza kumrejea kuwa kilichokatisha uhai wa Mwangosi kwa kuusambaratisha mwili wake, si risasi ya kawaida pengine ni mlipuko wa bomu kutokana na ukubwa wa kishindo chake.
Senga anasema baada ya tafakuri hiyo, hofu ya kibinadamu ikaanza kumpata, akijiona kuwa kumbe hata yeye hakuwa eneo salama kwake, akatamani kujificha kutokana na hofu kubwa aliyokuwa nayo.
Anasema alichofanikiwa kufanya baada ya kurudi katika hali ya kawaida, alirejea nyuma kama mita hamsini na kuuona ua uliojengwa kwa magome ya miti, akajibanza hapo huku machozi yakimtiririka akimlilia Mwangosi na kuongeza kuwa, hakuwa tena na hamu wala nguvu ya kushika kamera.
“Bado sikuamini na kuridhika na nilichokishudia kwa macho yangu mawili, niliendelea kuchungulia kujua nini kitaendelea. Ilichukua takribani dakika 15, askari hao wakikusanya mabaki ya mwili wa Mwangosi kwa kutumia ngao zao na kupakiza katika moja ya magari yao,” anaongeza.
Anasema baada ya zoezi hilo askari hao waliondoka, wakiwa ndani ya magari pamoja na baadhi ya viongozi, pia baadhi ya wafuasi waliokuwa wamewakamata kabla ya kuuawa kwa Mwangosi, wakielekea kusikojulikana.
“Mwenyezi Mungu ailaze pema roho ya marehemu Mwangosi. Amina,” anamaliza Senga.

Moja ya picha iliyopigwa na Senga ikionyesha askari Polisi (FFU) wakiwa kamili na zana zao
 CHANZO:GAZETI LA TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment