STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 19, 2012

Mawaziri watatu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wanatarajiwa kutumika kama mashahidi katika kesi ya kupinga matokeo

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar.
Mawaziri watatu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wanatarajiwa kutumika kama mashahidi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa Bububu, itakayofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chama hicho Issa Khamis Issa, katika Mahakama kuu ya Zanzibar.
Mawaziri hao watakaotoa ushahidi katika kesi hiyo, ni Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui na Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, ambao walikuwa waangalizi wa uchaguzi kupitia Chama cha Wananchi CUF.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar, Mkurugenzi wa habari, uenezi, haki za binadamu na mawasiliano na umma wa CUF, Salim Bimani alisema kwamba Mawaziri hao walishuhudia vitendo vya ukiukwaji wa taratibu na sheria za uchaguzi.
Bimani alisema hivi sasa jopo la wanasheria wanaendelea kukusanya vielelezo muhimu, kabla ya kufungua kesi wiki hii katika mahakama Kuu ya Zanzibar, na kuiomba kutengua ushindi wa mgombea wa CCM, Hussein Ibrahim Makungu, kwa madai kuwa ushindi wake haukutokana na maamuzi ya wananchi wa jimbo la Bububu.
"Katika kesi tutakayofungua, tutawatumia Mawaziri watatu kama mashahidi, kwa vile wameshuhudia kwa macho yao, vitendo vya udanganyifu, kuruhusiwa watu wasiohusika kupiga kura, na askari wa vikosi vya SMZ kutumia nguvu na kuwatisha wananchi katika zoezi hilo la uchaguzi mdogo wa Bububu.
Aidha, Bimani aliongeza kuwa kuna watu wawili wamejeruhiwa akiwemo Abdallah Haji Mmanga, anayedaiwa kupigwa risasi katika sehemu ya paja la mguu wake wa kulia, na Shah Haji Shah ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa na vigae vya chupa, ambao walitibiwa katika hospitali ya Al Rahma.
"Safari hii tumeamua kupambana kuanzia Mahakama kuu, na kama haki haitotendeka, tutafika katika Mahakam ya Rufaa, hatuwezi kuachia misingi ya demokrasia na utawala bora ikiendelea kuvunjwa chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa" alisema Bimani.
Alisema kwamba katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kuna viongozi bado wana dukuduku la maridhiano yaliyozaa Serikali hiyo, lakini kinyongo chao hakitofanikiwa kuzorotesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa au kuisambaratisha.
"Kuna viongozi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hawaungi mkono maridhiano, lakini Wazanzibari hatutaki kurejea katika malumbano ya kisiasa, hatua iliyofikiwa imeleta amani na utulivu katika nchi" alisema bimani
Hata hivyo, alisema kwamba uchaguzi wa Bububu hautopelekea Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuvunjika, kwa vile imekuja kutokana na maamuzi ya wananchi, ambao asilimia 66 waliunga mkono kuanzishwa kwa mfumo huo kupitia kura ya maoni iliypigwa 2010.
Alisema kwamba uchaguzi wa Bububu, Jeshi la Polisi lilishindwa kusimamia vyema majukumu yake na badala yake lilikasimu madaraka kwa vikosi vya SMZ ambavyo vilitumia vibaya majukumu yao na kushiriki katika vitendo vya kuwatisha wananchi kuweza kujitokeza na kupiga kura katika uchaguzi huo.
Bimani alisema CUF inalaani kitendo cha kupigwa kwa Mwandishi wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Munir Zakaria, kwa vile kimeingilia uhuru wake wa kikatiba wa kutekeleza majukumu yake ya kukusanya taarifa kwa ajili ya kuwahabarisha wananchi.
Alisema bahati mbaya tukio hilo limetokea siku chache tangu kuuwawa kwa Mwandishi wa Channel Ten mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, ambapo hakuna kiongozi dhamana wa Jeshi la polisi aliyewajibika kutokana na mauaji hayo ya kikatili.
Aidha aliongeza kuwa CUF imesikitishwa na kitendo cha kupewa masharti magumu ya dhamana kwa watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na vurugu za uchaguzi huo, ambapo kila mmoja alitakiwa kuweka dhamana ya shilingi laki tano kama fedha taslimu na dhamana ya maandishi 500,000 kwa kila mmoja kwa watuhumiwa 10 waliofikishwa katika mahakama ya mwanzo ya Mwanakwerekwe.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa jimbo la Mtoni ambaye ni mmoja kati ya watu waliopigwa katika vurugu hizo, Faki Haji Makame, alisema kwamba alipigwa mtama na kuanguka chini, wakati akiokota kiatu baada ya kumvuka alipokuwa akiwakimbia vijana waliomvamia na kumjeruhi.
"Mimi sijapigana hadharani, nimevamiwa na vijana wawili baadae akatokea mwengine, mnamhoji wa nini, wakati tumeagizwa apigwe, ndipo nilipoamua kukimbia na wakaanza kunifukuza na kunipiga" alisema Mbunge huyo wa jimbo la Mtoni.
Akielezea mukhtasari wa tukio lake, alisema kabla ya kushambuliwa wakati akitokea eneo la Kijichi, kukagua ujenzi wa nyumba yake, alipofika karibu na tawi la CCM eneo la Bububu, alimuona Naibu Katibu Mkuu wa CCm Zanzibar, Vuai Ali Vuai na kuamua kwenda kumsalimia, lakini alikataa kupokea salamu yake na kumshutumu kuwa CUF inazuia wafuasi wa CCM kwenda kupiga kura katika vituo.
"Alitahadharisha kuwa CCM haitokubali watu wake kunyimwa haki ya kupiga kura, na baada ya maneno yake, mimi nilianza safari ya kwenda kuwasalimia wakwe zangu katika eneo la Bububu, ndipo nilipokutwa na maswahiba ya kupigwa na kujeruhiwa kwa mwili wangu, kwa kunipiga kwa mipira ya mabomba ya maji na mateke na ngumi" alisema Mbunge huyo.
Alisema anakanusha taarifa ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa kuwa alikamatwa kwa madai ya kupigana hadharani, wakati Polisi ndio waliomuokoa alipokuwa akipigwa na kupelekwa katika kituo cha Bububu pamoja na watu waliokuwa wakimpiga.
Hata hivyo alisema jambo la kushangaza Polisi mpaka jana wameshindwa kumpa majina ya watu waliompiga, licha ya kuwa wamehojiwa, na vile vile wameshindwa kuwafikisha Mahakamani kutokana na makosa ya kumpiga na kumshambulia mwilini.
Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa CUF, Issa Khamis Issa, alisema kwamba ameshindwa kufungua kesi yake jana kama ilivyopangwa awali, kwa vile wanasheria wake wanaendelea kukamilisha vielelezo vitalkavyotumika kama ushahidi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo.
Alisema sheria ya tume ya uchaguzi inaeleza kuwa ndani ya siku 14, mgombea yeyote ana haki ya kupinga matokeo mahakamani endapo atakuwa hajaridhika na anatarajia kufungua kesi hiyo mapema wiki hii.
Wakati huo huo Mwandishi wa Channel Ten, Munir Zakaria ambaye alipigwa katika vurugu hizo za uchaguzi, ameendelea kupata matibabu, na afya yake inaendelea vizuri, baada ya kupigwa ngumi sehemu ya mdomoni na mabegani, lakini pochi iliyopotea ikiwa na vitu muhimu bado haijapatikana.
Alisema kwamba, tayari amekamilisha taratibu za matibabu katika hospitali ya Mnazi Mmoja, na anaamini watu waliomfanyia shambulia hilo watachukuliwa hatua za kisheria kwa vile tukio hilo limeripotiwa katika kituo cha Polisi cha Mwembe Madema mjini Zanzibar.
uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu ulifanyika Septemba 16 mwaka huu, ambapo ulitawaliwa na vurugu, uharibifu wa mali za umma, na matumizi mabaya ya silaha, hatua ambayo wadadisi wa mambo wameitafsri kuwa ni mwanzo mbaya wa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment