STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 4, 2011

Mwanza yaenguliwa Tamasha la Pasaka

MKOA wa Mwanza uliokuwa kwenye ratiba ya Tamasha la Pasaka, umeenguliwa na kufanya kwa sasa isalie mikoa mitatu tu itakayoshuhudia maonyesho hayo ya muziki wa Injili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama, alisema mikoa iliyosalia katika maonyesho hayo ni Dar es Salaam, Dodoma na Shinyanga.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Msama Promotions, alisema onyesho la kwanza la tamasha hilo litafanyika jijini Dar es Salaam siku ya April 24 kisha siku inayofuata litafanyikia mjini Dodoma kisha kumalizika Shinyanga Aprili 26.
Msama alisema onyesho la jiji la Mwanza limefutwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao na kuwaomba radhi mashabiki wa muziki wa Injili kwa jambo lililotokea.
"Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, tumefuta onyesho la jijini Mwanza na tunatanguliza kuomba radhi kwa lililotokea ambalo lilikuwa nje ya uwezo wetu, ila tunawahidi wale wa mikoa mingine watarajie burudani kabambe," alisema Msama.
Msama alisema onyesho la jijini litakalofanyika siku ya Sikukuu ya Pasaka litafanyikia kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo waimbaji nhyota wa muziki huo akiwemo Upendo Nkone na waimbaji toka mataifa mbalimbali ya Kiafrika watakuwepo ukumbini kutumbuiza.
"Onyesho la Dar na mengineyo yatapambwa na waimbaji nyota wa Tanzania na nchi jirani kama za Kenya, Uganda, Rwanda, DR Congo, Afrika Kusini na Zambia, lengo likiwa ni kukusanya fedha za kuwasaidia yatima na wajane," alisema Msama.
Aliongeza mbali na fedha hizo kuwanufaisha yatima na wajane kwa nia ya kujikumu na kupata mitaji ya kujiendeshea shughuli za biashara, pia sehemu ya mapato ya maonyesho hayo yatatolewa kwa waathirika wa mabomu yaliyotokea katika kambi ya jeshi Gongo la Mboto.
"Sehemu ya fedha zitakazopatikana kwenye maoanyesho hayo itatolewa kama pole kwa waathirika wa Mabomu ya Gongo la Mboto kama nilivyoahidi awali," alisema Msama.
Tamasha la Pasaka limekuwa likifanyika kila mwaka zaidi ya mwaka wa tatu sasa, ambapo waimbaji na makundi mbalimbali ya muziki wa Injili wa ndani ya nje hujumuika pamoja kutumbuiza sambamba na kuhamasisha upatikanaji wa fedha za kuwasaidia wenye matatizo nchini.

No comments:

Post a Comment