STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, March 8, 2011

Kaseba, Maugo kutambulishwa rasmi leo

MABONDIA Mada Maugo na Japhet Kaseba wanaotarajiwa kupigana Aprili 16, pamoja na watakaowasindikiza pambano hilo wanatarajiwa kutambulishwa rasmi leo mbele ya waandishi wa habari.
Mratibu wa pambano hilo, Kaike Siraju aliiambia Micharazo jana kuwa leo watafanya mkutano na vyombo vya habari kulitambulisha rasmi pambano hilo ambalo litafanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam.
"Nitawatambulisha rasmi mabondia wote watakaopigana Aprili 16 katika mkutano na vyombo vya habari utakaofanyika kesho (leo) kwenye ukumbi wa Habari-Maelezo majira ya saa 5," alisema Siraju.
Alisema katika mkutano huo, Maugo na Kaseba kila mmoja atapata fursa ya kuongea machache kuhusiana na pambano lao hilo la raundi nane uzito wa kilo 72 litakalokuwa la kusaka mkali baina yao wa kuzipiga na Francis Cheka.
Ingawa Siraju amekuwa akificha majina ya mabondia watakaoshindikiza pambano hilo, lakini uchunguzi wa Micharazo umebaini kuwa nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya ngumi ya ridhaa, Joseph Martin ni miongoni mwao.
Martin aliyeachana na ngumi za ridhaa na kuingia za kulipwa atapigana na Sweet Kalulu, pia Francis Miyeyusho na Afande Juma nao watakuwepo katika usindikizaji.
Kwa mujibu wa Siraju, mgeni rasmi wa pambano hilo anatarajiwa kuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ambaye atamualika IGP Said Mwema kuhudhuria kwenye ngumi hizo.

No comments:

Post a Comment