STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, March 8, 2011

Msamba 'ajitoa' Villa Squad *Ni baada ya kuirejesha Ligi Kuu

KOCHA aliyeipandisha daraja klabu ya Villa Squad hadi Ligi Kuu Tanzania Bara, Abdallah Msamba, ametangaza 'kuitema' timu hiyo akiutaka uongozi usake kocha mwingine wa kuiongoza kwenye ligi hiyo msimu wa 2011-2012.
Akizungumza na Micharazo, Msamba, alisema baada ya kutimiza jukumu la kuirejesha Ligi Kuu, Villa Squad anaona ni vema kupisha kocha mwingine wa kuendelea kuinoa timu hiyo katika ligi hiyo msimu ujao.
Msamba, alisema kujiondoa kwake kuinoa timu hiyo haina maana kuwa kajitoa kabisa Villa Squad, ila alisema kwa hadhi ya ligi ilivyo inapaswa timu iwe na mtu mwingine kukabiliana na mshikemshike wake.
"Nimeashautaarifu uongozi utafute kocha mwingine wa kuiandaa timu kwa ligi kuu ijayo, mie naishia hapa baada ya kuipandisha daraja, ila nitakuwa kocha msaidizi au mshauri kwa lengo la kuona Villa inafanya vema," alisema.
Winga huyo wa zamani wa Sigara, Simba na Kajumulo World Soccer, alisema ili kuweza kufanya vema kwenye ligi hiyo, Villa inahitaji kufanya marekebisho kidogo katika kikosi chake, chini ya kocha mwenye hadhi stahiki.
Alisema ana imani kama marekebisho hayo yatafanyika mapema na timu kuandaliwa mapema ikipata michezo mingi ya kujipima nguvu inaweza kutisha katika ligi hiyo iliyowahi kuicheza kabla ya kushuka msimu wa 2008-2009.
Villa Squad ni miongoni mwa timu nne zilizopanda Ligi Kuu msimu ujao baada ya kufanya vema kwenye Ligi Daraja la Kwanza iliyochezwa mjini Tanga.
Timu zingine zilizoungana na klabu hiyo yenye maskani yake Magomeni Mapipa ni JKT Oljoro waliokuwa mabingwa wa ligi hiyo ya daraja la kwanza, Coasta Union na Moro United zinazorejea tena kwenye Ligi Kuu ya Tanzania.

Mwisho

No comments:

Post a Comment