STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 23, 2010

Aisha Sururu ataka umoja jumuiya za Kiislam

MWENYEKITI wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania, BAKWATA, Aisha Sururu, ameziomba taasisi za Kiislam nchini kushikamana na kuombea uchaguzi mkuu uwe wa amani na utulivu.
Sururu, ambaye ni mgombea wa udiwani wa Viti Maalum CCM, alisema umoja na mshikamano ndio silaha pekee ya kuifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya amani na utulivu na kuzikumbusha jumuiya hizo Kiislama kuidumisha.
Mwenyekiti huyo aliyasema hayo alipozungumza na Micharazo jana jijini Dar es Salaam na kudai taasisi na jumuiya hizo zina wajibu mkubwa wa kuwa mfano kwa wengine kwa kuwa na umoja na mshikamano bila kubaguana.
Alisema kujumika pamoja kwa viongozi na wafuasi wa jumuiya mbalimbali za kiislam katika hafla ya ufuturishwaji futari uliofanywa na Taasisi ya Al Madinah ni moja ya dalili njema za umoja miongoni mwao aliotaka udumishwe milele.
Alisema umoja huo hautafaa kama hawatashirikiana kwa ajili ya kuiombea nchi kufanya uchaguzi mkuu Oktoba 31 kwa amani na utulivu ili kuendeleza hali ya utilivu iliyopo nchini kwa miaka mingi.
"Kama kiongozi wa jumuiya ya wanawake ya BAKWATA nilikuwa nahimiza umoja na mshikamano kwa jumuiya zingine kuiombea Tanzania ifanye uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu ili tuishi na raha mustarehe," alisema.
Sururu, alisema kwa kuwa lengo la kila Mtanzania ni kuona amani na utulivu unaendelea kudumu basi ni vema wananchi wakashikamana na kutokubali kuwaachia wachache wawavuruge kwani majuto yake ni makubwa baadae.
Aliongeza kuwa, pamoja na kuhimiza umoja huo, pia anawaomba wananchi waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 31 kuchagua viongozi wanaowataka na kuwaamini kwa mustakabali wa nchi na maisha yao kwa ujumla.
Juu ya wagombea waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo, Sururu aliwataka wafanye kampeni za kistaarabu kwa kumwaga sera zao ili kuwashawishi wananchi wawapigie kura siku ya kufanya hivyo.
Hafla hiyo ya kufuturishwa kwa wanawake wa Kiislam ilidhaminiwa na Benki ya Stanbic
Mwisho

No comments:

Post a Comment