STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 22, 2010

Wagombea Kilosa kuanza kampeni Agosti 26





WAGOMBEA wa CCM wanaowania viti vya Ubunge na Udiwani wilaya ya Kilosa wanatarajia kuanza rasmi kampeni zao Agosti 26 mwaka huu, wakati mgombea wao wa Urais, Rais Jakaya Kikwete atakapoenda kuzindua kampeni hizo jimbo la Mikumi.
Katibu wa CCM-Kilosa, Gervase Makoye, alisema wagombea wa CCM wataanza kampeni zao rasmi siku hiyo wakati rais atakapozuru Mikumi kuendelea kujikampenia kuomba kura za wananchi kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31.
Makoye alisema, wagombea wote watatu wa majimbo matatu yaliyopo wilayani kwao watahudhuria kampeni hiyo kabla ya kila mmoja kutawanyika jimboni mwake kuanza kuomba kura za wananchi wa maeneo yao.
Katibu huyo alisema baada ya Rais kuzindua Mikumi Agosti 26, siku inayofuata atakuwa Kilosa kisha kumalizia Gairo na kuwaacha wagombea wahusika wakiendelea na kampeni zao.
Jimbo hilo la Mikumi linawaniwa na Abdulsalaam Nahad Suleiman 'SAS', ambaye alisema amejipanga kuhakikisha anaibuka kidedea kwenye kinyang'anyiro hicho kinachowaniwa na wagombea wengine wa vyama vya mbalimbali vya upinzani.
Naye mgombea wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkullo alisema yeye ataanza rasmi kampeni zake Agosti 27 baada ya Rais kuzindua kampeni za wilaya hiyo huko Mikumi na hapo ndipo atakapoanika kila kitu juu ya ukweli kuhusu alichowafanyia wakazi wa jimbo hilo na yale ambayo amepania kuyaendelea na kufanya mengine mapya.
Mkullo alisema mbali na hilo, lakini pia atazitumia siku 70 za kampeni hizo kuweka bayana juu ya tuhuma dhidi yake kuwa yeye sio raia wa Tanzania bali ni Mmalawi, madai aliyodai yametolewa na mmoja wa waliokuwa wagombea wenzake asiyekubali matokeo.
"Kampeni zangu nitazianza Agosti 27 na hapo ndipo nitapata fursa nzuri ya kusema kila kitu juu ya mipango yangu ya maendeleo kwa wakazi wa jimbo langu na pia kuweka hadharani madai juu ya tuhuma za utata wa uraia wangu," alisema Mkullo.
Mgombea wa Gairo, Ahmed Shabiby, yeye alisema yupo vema na atajinadi ili kuomba ridhaa ya wakazi wa jimbo hilo kumpa tena nafasi ya kuwatumikia kama walivyompa katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2005.

No comments:

Post a Comment