STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 1, 2012

LEO NDIO LEO FAINALI ZA UERO 2012

MABINGWA watetezi wa Kombe la nchi za Ulaya, Hispania leo inatarajiwa kushuka dimbani kujaribu kuendeleza rekodi yake katika michuano ya kimataifa kwa kuvaana na Waitalia. Timu hizo mbili zilizofuzu fainali za mwaka huu za barani humo, zitaavanaa kila moja ikitaka kudhihirisha ubabe wake baada ya mechi yao ya awali ya makundi kuisha 1-1. Baina ya nchi hizo Hispania na Italia zimetoa mabingwa 25 wa Ulaya katika ngazi ya klabu lakini hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu zao za taifa kukutana katika fainali ya kombe la Mataifa ya Ulaya. Ni wachache watahoji uhalali wa timu hizo kufika fainali. "Mshindi atakuwa bingwa anayestahili," alisema kiungo wa Hispania Cesc Fabregas. "Nadhani timu hizi mbili ndiyo zimekuwa na matokeo mazuri mfululizo katika michuano hii." Italia ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia, mara ya mwisho 2006, wakati Hispania inajaribu kufanya kitu cha kipekee kwa kuwa timu ya kwanza kutwaa mfululizo vikombe vitatu vikubwa baada ya Euro 2008 na Kombe la Dunia miaka miwili iliyopita. Wakati mafanikio ya Vicente Del Bosque na Hispania yamejengwa katika safu imara ya ulinzi na kukaa muda mrefu na mpira, Italia imefika fainali kutokana na kufanya mashambulizi mfululizo yakiongozwa na mtukutu Mario Balotelli ambayo yaliiwezesha kuitoa Ujerumani katika nusufainali. Mfumo wa Hispania, wa pasi fupi-fupi 'Tiki Taka' umewapa mafanikio ya kujivunia - hakuna timu ya Ulaya tangu Ujerumani Magharibi mwanzoni mwa miaka ya 1970 imefanikiwa kucheza fainali tatu mfululizo za michuano mikubwa. Lakini 'enzi ya Hispania' kwa namna nyingi itaelezewa na jinsi itakavyokabiliana na timu iliyoshangaza kwa kucheza soka la kuvutia ya Italia leo. Kuweka historia ya kutwaa taji la tatu mfululizo, huku vigogo Ujerumani na Uholanzi vikiwa vilishafunga virago kwenye fainali hizi, kutaiweka Hispania kama moja ya timu kabambe zaidi zilizowahi kutokea. Lakini kipigo, mwishoni mwa fainali ambazo wameshindwa kuchengua mashabiki, kutaendelea kuitambulisha 'La Roja' kama moja ya timu za kawaida miongoni mwa vigogo vya soka. Hispania imefika hatua hiyo ya fainali kwa kuiondosha kwa mikwaju ya penati 4-2 wareno wakiongozwa na nahodha wao Cristiano Ronaldo, huku Waitalia maarufu kama 'Azzurri' waliwanyamazisha waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuwa mabingwa wa mwaka huu, Ujerumani kwa mabao 2-1, magoli yaliyofungwa na 'mtukutu' Mario 'Super Mario' Balotelli ambaye ana asili ya Afrika hususani nchini Ghana.

No comments:

Post a Comment