STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 16, 2010

Extra Bongo yawanyatia akina Chokoraa





BAADA ya bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kuwatimua kundini, wanamuziki wao nyota wawili, Khalid Chokoraa na Kalala Junior, uongozi wa bendi ya Extra Bongo, umeanza mipango ya kuwachukua wanamuziki hao kuimarisha kikosi chao.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki, aliiambia MICHARAZO kuwa, tayari wameshaanza mazungumzo ya awali na wanamuziki hao ambao pia wanaunda kundi la Mapacha Watatu wakishirikiana na Jose Mara wa FM Academia.
Choki alisema walikuwa na mipango ya kuwachukua waimbaji hao kitambo kirefu,ila walikuwa wakisita kuhofia kutifuana na uongozi wa Twanga Pepeta, lakini kutimuliwea kwao kwa utovu wa nidhamu ni kama kumewarahisishia kazi.
"Kutimuliwa kwao Twanga Pepeta kumeturahisishia kazi ya kuwapata waimbaji hawa wenye vipaji vya aina yake na tumeshaanza mazungumzo ya awali, nadhani ndani ya wiki hii mambo yatakuwa shwari na wataanza kazi Extra Bongo," alisema Choki.
Choki aliongeza katika kuonyesha kuwa wapo karibu na wanamuziki hao na kuwakubali kwa kazi zao kupitia kundi lao la Mapacha watatu wanatarajia kufanya nazo onyesho la pamoja wakati wa Mkesha wa Mwaka Mpya na siku ya Mwaka Mpya wenyewe jijini Dar es Salaam.
Alisema onyesho la kwanza baina yao na Mapacha Watatu linalotamba na albamu ya 'Jasho la Mtu' litafanyika mkesha wa Mwaka Mpya, Vatican Hotel, Sinza na kisha siku ya Mwaka Mpya watakuwa wote pale TCC Chang'ombe.
"huwezi jua kwenye maonyesho hayo mawili yanaweza kutumiwa kama utambulisho wao ndani ya Extra Bongo," Choki alitania.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, lengo la bendi yao ni kutaka kuona wanatamba kwenye muziki wa dansi nchini baada ya kurejea kwa mara ya pili baada ya kufariki enzi ikitumia miondoko ya 3x3.
Choki aliongeza wakati wakiwa, katika harakati hizo za kuwanyakua akina Chokoraa, aliyekuwa mmoja wa waasisi wa Extra Bongo ya awali, pia bendi yao inajiandaa kufanya uzinduzi wa albamu ya 'Mjini Mipango'.
Alisema uzinduzi uliofanyika Mei 25 mwaka huu ulikuwa ni wa bendi yao iliyofufuliwa upya na sio wa albamu kama baadhi ya watu walivyokuwa wanadhani na hivyo wanajipanga kuifanyia uzinduzi wake.
Choki alisema watazindua albamu hiyo yenye nyimbo sita ambazo baadhi zinaendelea kutamba kwenye vituo vya redio na runinga, huku wakiendelea kuandaa ya pili ambayo tayari baadhi ya nyimbo zake zimeshakamilika.

No comments:

Post a Comment