STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 15, 2011

Stars kukipiga ughaibuni na Palestina, Jordan

KATIKA kujiweka fiti kabla ya kumaliza viporo vya michezo yake miwili iliyosalia ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika za mwaka 2012, timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kwenda Mashariki na Kati kucheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuopitia Afisa Habari wake, Boniface Wambura inasema, Stars itaumana na timu za mataifa ya Palestina na Jordan mapema mwezi ujao.
Wambura alisema mechi ya kwanza ya timu hiyo inayoshikilia nafasi ya tatu katika kundi D lenye timu za Morocco, Afrika ya Kati na Algeria, itachezwa siku ya Agosti 10 katika mji wa Ramallah dhidi ya wenyeji wao Palestina.
Mechi ya Tanzania na Palestina itakuwa ni kama marudiano, kwani mapema mwaka huu timu hizo zilipepetana hapa nchini katika pambano jingine la kirafiki la kimataifa.
Katika mechi hiyo ilichezwa Februari 9 kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Stars iliitambia Palestina kwa kuilaza bao 1-0, bado lililofungwa na winga mahiri, Mrisho Ngassa ambaye kwa sasa yupo Marekani kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Seattle Sounders inayoshiriki ligi ya Marekani, MLS.
Wambura aliongeza Stars itashuka tena dimbani Agosti 13 kupepetana na Jordan katika pambano litakalochezwa kwenye mji mkuu wa nchi hiyo ya Jordan, Amani.
Wambura alisema Stars itaondoka nchini Agosti 7 na kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kutajwa mara baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen kurejea kutoka mapumziko nchini Denmark, mapema mwezi ujao.
Stars inahitaji ushindi katika mechi zake zilizosalia dhidi ya Algeria itakayochezwa nyumbani na ile ya mwisho dhidi ya Morocco, iwapo inataka kufuzu fainali hizo za Afrika zitakazofanyika mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.

No comments:

Post a Comment