STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 15, 2011

Ndolo, Fabriges wagonganisha vichwa Yanga


PANGA pangua ya nani abaki na yupo atoke kati ya Tonny Ndolo na Haruna Niyonzima 'Iniesta' ndani ya usajili mpya wa mabingwa wapya wa Kombe la Kagame, Yanga, imeibua mzozo ndani ya klabu hiyo.
Ndolo, Mganda aliyesajiliwa toka Kagara Sugar na Iniesta aliyetoka APR ya Rwanda, mmoja kati yao anapaswa kuachwa kwenye usajili ili kutekelezwa kwa kanuni ya idadi ya wachezaji wa kigeni wanaopaswa kusajiliwa na klabu za soka nchini.
Yanga tayari imetimiza idadi ya wachezaji sita wa kigeni, mmoja zaidi ya idadi inayotakiwa na TFF na kwa maana hiyo kuilazimisha klabu hiyo kupunguza jina moja na mzozo unakuja juu ya nani aachwe kati ya wachezaji hao wawili kutokana umuhimu wao katika kikosi hicho.
Awali ilikuwa ikitajwa kwamba mshambuliaji Hamis Kiza 'Diego' ndiye aliyekuwa katika hatihati ya kubakishwa Yanga, lakini kwa kiwango alichokionyesha kwenye michuano ya Kagame akiifungia mabao muhimu akishirikiana na 'mapro' wengine wawili, Davis Mwape wa Zambia na Kenneth Asamoah aliyewapa ubingwa mbele ya Simba, hali imekuwa kizungumkuti.
Mchezaji mwingine wa kigeni aliyepo Yanga ni kipa Yew Berko kutoka Ghana ambaye msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara alichaguliwa kuwa Kipa Bora akimfunika Juma Kaseja.
Habari za ndani za klabu hiyo zinasema mapendekezo ya kocha Sam Timbe tangu awali ni kuachana na Iniesta, lakini kamati ya usajili imekuwa ikimkumbatia kiungo huyo, ikitaka wa kuachwa awe Ndolo, kitu ambacho kocha hataki kusikia kutokana na kumhitaji nyota huyo.
Hali hiyo imefanya hata Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu kushindwa kujua ukweli yupi kati ya wachezaji hao wawili ndiye atakayeachwa wakati dirisha la uhamisho wa wachezaji likifungwa Alhamisi iliyopita.
"Kwa kweli mie sijui nani ataachwa, ila hatma yao itafahamika wakati wowote kwa vile tunajua tunatakiwa kupunguza jina la mchezaji mmoja kutokana na kuzidisha idadi ya wachezaji wa kigeni inayotakiwa na kanuni za usajili nchini," alisema Sendeu.

No comments:

Post a Comment