STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 15, 2011

Wafanyakazi wa Majumbani sasa wapata 'Rungu'

KUPITISHWA kwa Mkataba wa Kimataifa wa 189 wa Shirika la Kazi Duniani, ILO,
kumeelezwa kuwa kama ni 'rungu' kwa wafanyakazi wa majumbani kuwashughulikia waajiri
wao watakaokiuka sheria na mikataba ya kazi kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine nchini.
Mkataba huo wa kuwatambua wafanyakazi hao wa majumbani ulipitishwa Juni 16 mwaka huu
katika mkutano wa 100 wa ILO uliofanyika nchini Uswisi, ambapo siku moja kabla ya
kupitishwa kwake, Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alihutubia mkutano huo kuuridhia,
Akizungumza na MICHARAZO, Mratibu wa Shirika la Wafanyakazi wa Majumbani Kanda ya
Afrika, IUF, Bi Vick Kanyoka, alisema kuridhiwa kwa mkataba huo kumetoa fursa na nafuu kwa watumishi hao wa majumbani ambao kwa miaka mingi walikuwa hawathaminiwi nchini.
Bi Kanyoka, alisema kulingana na mkataba huo ni kwamba wafanyakazi wa majumbani kwa
sasa wanatambuliwa kama wafanyakazi wengine wakihitajiwa kulindwa na kupewa haki zao
ikiwemo kusainishwa mikataba na makubaliano kabla ya kuanza kazi kwa muajiriwa.
Mratibu huyo alisema kitu cha muhimu baada ya kupitishwa kwa mkataba huo ni serikali ya Tanzania na wananchi wake kuutekeleza kwa vitendo mkataba huo ili kuhakikisha wafanyakazi wanajivunia kazi yao tofauti na siku za nyuma walipokuwa wakijificha.
"Kwa hakika kupitishwa kwa mkataba huo wa 189 ni kama rungu kwa wafanyakazi wa
majumbani kuweza kuwabana waajiri wao, ambao kwa miaka mingi walikuwa wakiwabagua,
kuwanyanyasa na kuwadharau wakiwachukulia kama 'vijakazi'," alisema.
Aliongeza kwa kuwataka watumishi hao kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa mkataba huo kwa kutokubali kuajiriwa kabla ya kuingia mkataba na kuridhia haki zake stahiki katika ajira yake, ili inapotokea tatizo mbele ya safari iwe rahisi kusaidiwa.
Bi Kanyoka, aliwasihi pia waajiri kuridhia na kuutekeleza mkataba huo kwa kuamini watumishi hao ni kama sehemu za familia zao na hivyo kuwapa huduma na stahiki zote ikiwemo kuwalipa fedha kulingana na kima wanachokubaliana na kwa muda muafaka.
"Pia wawajali na kuwathamini kwa sababu wao ni watu tegemeo kwao na familia zao, hivyo kukaa nao kwa ubaya ni kusababisha matatizo ambayo tumekuwa tukishuhudia katika jamii yetu," alisema.
Mratibu huyo alisema mkataba huo ulipitishwa kwa kupigiwa kura 396 za ndio huku kura 16 zikiukataa miongoni mwa nchi zilizougomea ikiwa ni taifa la Uingereza, huku mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania na yale ya Amerika Kusini na Kaskazini yakiongoza kwa kuupitisha.

No comments:

Post a Comment