STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 24, 2014

Rais wa TPBO, Ustaadh Yasin 'aula' Afrika Mashariki na Kati


RAIS wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited) Yasin Abdallah 'Ustaadh' (pichani) ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa la Afrika Mashariki na Kati (ECAPBA).
Kwa mujibu wa taarifa ya Rais wa ECAPBA ambaye pia ni Rais wa IBF-USBA, Onesmo Ngowi uteuzi umefanywa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo la ECAPBA kilichofanyika Januari 4 mwaka huu jijini Kigali, Rwanda kilichofanya mabadiliko ya kujaza nafasi za uongozi wa shirikisho lao.
Ngowi alisema Ustaadh amechukua nafasi  kuchukua nafasi ya Celestino Mindra kutoka Uganda aliyekuwa Rais wa Baraza la Ngumi za Kulipwa za nchi hiyo (UPBC).
Mbali na Ustaadh wengine walioteuliwa kwenye kikao hicho ni Simon Kategole wa Uganda, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa ECAPBA kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Shaaban Ogolla wa Kenya ambaye yuko masomoni nchini Marekani.
Pia Daudi Chikwanje wa Malawi anachukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa ECAPBA, huku Nelson Sapi wa Zambia ameteuliwa kuwa Naibu Mweka Hazina wa ECAPBA akimsaidia Nemes Kavishe wa Tanzania.
Boniface Wambura wa Tanzania amebaki katika nafasi yake ya Afisa Habari wa ECAPBA wakati wajumbe wanne wameongezwa kwenye Kamati ya Utendaji ambao ni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Malawi na Ethiopia pamoja na Roman Chuwa wa Arusha.
Aidha, ECAPBF imemshukuru Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Gaudence Lyimo kwa kukubali kuwa mlezi wake na kuipatia ofisi katika Manispaa ya jiji la Arusha kikiwa ndicho Chombo cha michezo kinachounganisha vijana cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
"Katika malengo yake, ECAPBA itafanya kazi kwa karibu sana na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) ili iweze kuwa chachu ya utekelezaji wa maamuzi ya Jumuiya katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati," taarifa hiyo ya Ngowi inasema na kuongeza.
"Kwa kutambua kuwa, Jumuiya ya Afrika ya Mashariku ni chombo cha uchumi cha kuunganisha nguvu za watu wa Afrika ya Mashariki, ECAPBA imedhamiria kuyafanyia utekelezaji maamuzi yote yanayohusu maendeleo ya vijana pamoja na ushirikiano wa utamaduni na michezo wa EAC. Aidha, ECAPBA imedhamiria kuleta chachu katika kujenga nguvu na kutengeneza ajira kwa vijana wa Afrika ya Mashariki na Kati."

No comments:

Post a Comment