STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 24, 2014

Ushindani wa namba Simba wamkuna Ali Badru


USHINDANI wa kugombea namba kwa wachezaji wa Simba umemkosha mshambuliaji mpya wa klabu hiyo, Ali Badru, akisema utaisaidia timu yao kuwa kali zaidi kwenye duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara inayoanza kesho.
Akizungumza na MICHARAZO, Badru alisema mpaka sasa ndani ya Simba hakuna mwenye uhakika wa namba, kitu ambacho kinawafanya wachezaji wasilale ili kupigania kupata nafasi chini ya kocha Zdravko Logarusic anayeinoa timu hiyo.
Badru aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo akitokea nchini Misri, alisema kama mchezaji anayejitambua, anafurahia hali ya ushindani wa kugombea namba baina yake na wachezaji wenzake akiamini ni nafasi ya kuonyesha uwezo aliojaliwa.
"Kwa kweli nafurahishwa na ushindani wa namba uliopo Simba, unatufanya wachezaji wote kuwa macho na kuongeza bidii ili kuwaridhisha makocha na hali hii inasaidia kuongeza viwango vyetu," anasema.
Badru anayeichezea timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), alimmwagia sifa kocha Logarusic kwamba ni 'bonge' la kocha kuwahi kumfundisha soka na kuitabiria Simba kufika mbali chini ya mtaalam huyo kutoka Croatia.
"Siyo siri nimefundishwa na makocha mbalimbali, lakini kati yao sijaona kama Loga, huyu jamaa ni bonge la kocha na kama atadumu na klabu naamini Simba itafika mbali, anajua kazi yake na anahamasisha sana wachezaji kujituma," alisema.
Simba iliyomaliza duru la kwanza la ligi chini ya kocha aliyetimuliwa Abdallah Kibadeni na kushika nafasi ya nne, itaanza kibarua cha duru la pili siku ya Jumapili kwa kuikaribisha Rhino Rangers ya Tabora kwenye uwanja wa Taifa.
Katika pambano lao la awali lililochezwa kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.

No comments:

Post a Comment