STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 1, 2015

Arsenal, Manchester City vitani tena EPL

WAKIWA na maumivu ya vipigo walivyopata kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, klabu za Arsenal na Manchester City zitakuwa tena vitani leo kwenye viwanja tofauti katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Arsenal walikandikwa mabao 3-1 na Monaco ya Ufaransa itakuwa nyumbani kuumana na Everton, wakati Manchester City watakuwa wageni uwanja wa Anfield kupepetana na Liverpool.
Mabingwa watetezi hao walikumbana na kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Barcelona, na leo watakuwa na kazi ngumu mbele ya Liverpool ambayo imekuwa na matokeo ya kuvutia siku za karibuni.
Katika mechi nne zilizopita za ligi hiyo, Liverpool haijapoteza mchezo wowote, pia ikishinda katika Kombe la Ligi na Ligi Ndogo ya Ulaya.
Zilipokutana mara ya mwisho Agosti 25 mwaka jana katika mechi ya mkondo wa kwanza Liverpool ilinyooshwa na Manchester City kwa mabao 3-1 ugenini hivyo leo kulazimika kulipa kisasi kwa wageni wao.
Kocha wa Man City, Manuel Pellegrini amesisitiza umuhimu wa kupata ushindi katika mchezo huo wa ugenini ili kuweza kupunguza pengo la pointi dhidi ya Chelsea wanaoongoza msimamo wakiwa na pointi 60.
Katika mechi itakayochezwa Emirates, Arsenal itavaana na Everton ambayo katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa Agosti 23 mwaka timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutosa sare ya mabao 2-2.
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger aliyewashutumu vijana wake kwa kipigo cha Monaco atakuwa na kazi ngumu ya kuwaongoza kikosi chake kupata ushindi nyumbani ili angalau kuwafukuzia Man City.
Wenger anatambua ni michuano miwili tu mpaka sasa ndiyo wana hakika ya kutwaa taji kama watakomaa, Kombe la FA wanaotetea na watakaovaana naManchester United wiki ijayo na michuano ya ligi.
Nafasi ya kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ni finyu baada ya kipigo cha Monaco wakilazimika kuhakikisha wapate ushindi wa 3-0 wiki mbili zijazo nchini Ufaransa.
Everton wenyewe wamekuwa na mwenendo wa kuchechemea msimu huu, ingawa siyo timu ya kubezwa kwani inaweza kufanya lolote katika pambano hilo la leo.

No comments:

Post a Comment