STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 6, 2013

Kinondoni yainyuka Pwani 7-0 Copa Coca Cola


MABINGWA mara mbili wa Copa Coca-Cola timu ya Kinondoni imewapa kipigo kikubwa wenyeji timu ya Pwani cha magoli 7-0 katika mashindano yanayoendelea ya vijana chini ya umri wa miaka 15 ya Copa Coca-Cola ngazi ya kanda kwenye uwanja wa Tumbi, Kibaha juzi jioni.
Kinondoni walipata goli lao la kwanza katika dakika ya 4 kupitia kwa Kidanga Hamadi baada ya kuunganisha krosi kutoka upande wa kulia. Hamadi kwa mara ya pili alitikisa nyavu za wapinzani wao katika dakika ya 11 baada ya kuwapiga chenga mabeki wa timu ya Pwani na kupiga shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.
Magoli mengine yalifungwa na Alex Milanzi katika dakika ya sita, Oswin Nungu katika dakika ya 20, Ayubu M. Ayubu katika dakika ya 41, Majid Musa katika dakika ya 66 kwa njia ya penati na Aboubakari Mussa alihitimisha karamu ya magoli katika dakika ya 74.
Katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza, Geita waliifunga Mara 1-0 katika mechi iliyojaa ushindani.
Kigoma hawakuwa na bahati siku ya Jumatano baada ya kupoteza mchezo dhidi ya wenyeji timu ya Mwanza kwa kufungwa  2-1. Beki wa Kigoma, Hashimu Mussa alijifunga mara mbili katika dakika ya kwanza na ya 72. Kigoma walipata goli lao katika dakika ya 36 kupitia kwa Rashidi Bakari.
Mechi nyingine iliyochezwa katika uwanja huo wa chuo cha ualimu Butimba, Tabora waliilaza Simiyu 2-1. Tabora  walipata goli la kwanza katika dakika ya sita kupitia kwa Selemani Husein kwa njia ya penati kabla ya Rashidi Omary kuhitimisha katika dakika ya 54.
Mechi nyingine katika uwanja wa Butimba juzi iliwakutanisha Shinyanga na Kagera ambapo Shinyanga walishinda 3-0. Magoli ya Shinyanga yalipachikwa wavuni na Anwar Amada katika dakika ya 24, Jahid Nuru dakika ya 60 na Felix Rweyemamu dakika ya 74.
Katika uwanja wa Mkokotoni , Zanzibar , Timu ya Kaskazini Pemba na Kusini Unguja walitoka sare ya 3-3 wakati huo huo Tanga na Temeke nao walitoka sare ya 4-4. Na katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Singida  waliilaza Manyara kwa mabao 2-0.
Fainali za Taifa za Copa Coca-Cola zinahusisha timu 16 ambazo zitaanza kuchuana wiki ijayo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment