Waumini wa Kiislam wakiwa kwenye ibada ya swala |
WAKATI mwezi mtukufu wa Ramadhani ukikaribia kuanza, nchini Uingereza kituo kimoja cha runinga kimetangaza kuanza kurushwa hewani moja kwa moja adhana ya swala ya asubuhi.
Chaneli ya 4 ya televisheni nchini humo, imesema itaanza kurushwa hewani adhana hiyo ya asubuhi 'live' kuwaamsha waumini wa kiislam ili kuwahi swala.
Justine Bower mkurugenzi wa masuala ya umma wa chaneli ya 4 ya televisheni ya nchi hiyo amesema kuwa, kanali hiyo itakuwa ikirusha moja kwa moja adhana ya asubuhi kwa ajili ya wananchi wa Uingereza. Ameongeza kuwa, waumini wa dini ya Kiislamu wapatao milioni mbili na laki nane nchini humo wataanza mfunguo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani siku chache zijazo.
Bower amesema kuwa kanali hiyo pia itakuwa ikirusha hewani adhana kupitia mtandao wa kanali hiyo.
Alipoulizwa wamejiandaa vipi kukabiliana na ukosoaji kwa hatua hiyo, Justine Bower amesema kuwa, karibu asilimia 5 ya wananchi wa nchi hiyo wako katika pilika pilika za kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Amesema kuwa, mwezi wa Ramadhani hufungwa na waumini wa dini ya Kiislamu kila mwaka, na nitawashangaa watu watakaostaajabishwa na uwepo wa utambulisho huo wa kidini.
Mfungo huo ambao unatarajiwa kuanza kati ya Julai 8 na 9 ni kati ya nguzo tano za dini ya kiislam ambapo waumini hujizuia kula na kunywa mchana pamoja na kujikithirisha kufanya mambo mema kwa nia ya kutaka radhi za Allah Subhana Wataala.
(Radio Tehran via Wavuti)
No comments:
Post a Comment