STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 12, 2012

Pambano la watani wa jadi Msondo wajichimbia Dodoma, Sikinde wajificha

HOMA ya pambano la wapinzani wa jadi kwenye muziki wa dansi nchini kati ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' na Mlimani Park 'Sikinde' linalotarajiwa kufanyika Idd Mosi kwenye viwanja vya Leaders Club limechukua sura mpya baada ya bendi mmoja kukimbia mji na nyingine kwenda kusikojulikana. Bendi ya Msondo imelikimbia jiji la Dar es Salaam na kwenda kujichimbia mkoani Dodoma kujiandaa kikamilifu na pambano hilo la aina yake dhidi ya mahasimu wao. Meneja wa bendi hiyo Said Kibiriti amesema kuwa bendi iko Dodoma ikifanya mazoezi ya 'kufa mtu' ili kuwatoa nishai Sikinde na wasiwe na hamu tena ya kuomba pambano siku nyingine. "Tunataka tutoe dozi siku hiyo, tutawasambaratisha na waogope tena kupambana na sisi, mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi bendi yetu iko sawa na sasa inajifua na siku ya Idd El Fitri wajitokeze kwa wingi kuja kuishangilia Msondo," alisema Kibiriti. Kwa upande wa Sikinde, kiongozi wa bendi hiyo Habib Jeff amesema kuwa bendi yao ipo jijini Dar es Salaam, lakini akagoma kabisa kutaja sehemu ilipojichimbia. "Ndugu yangu sisi tupo hapa hapa Dar, ila siwezi kukwambia tupo wapi, tunaogopa hujuma, si unajua tena linapokuja suala la Msondo na Sikinde ni kama Simba na Yanga kwa hiyo mashabiki watatuona tu siku siku hiyo, wala hatusemi kwa sasa yuko wapi ila hapa hapa Dar," alisema. Kiongozi huyo amewataka mashabiki wake kujazana kwa wingi siku ya Idd Mosi kwenye viwanja vya Leaders Club kuipa sapoti bendi yao ili iibwage Msondo. Pambano hilo limeandaliwa na kampuni ya Keen Arts na kudhaminiwa na Konyagi. Bendi hizo zilipambana kwenye sikukuu ya Krisimasi mwaka jana kwenye ukumbi wa TCC. Mwisho

No comments:

Post a Comment