STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 3, 2012

Okwi afuzu majaribio yake Austria

MSHAMBULIAJI tegemeo wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba, Emmanuel Okwi amefuzu majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Redbull Salzburg ya nchini Austria alikoenda kwa majaribio ya wiki mbili, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema jana. Hata hivyo, Okwi ambaye hakuwepo wakati Simba ikiishia robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), atarejea nchini wakati wowote ili kutibiwa malaria ambayo inamsumbua tangu alipotua Austria, alisema Kaburu. Aliongeza kuwa Simba inatarajia kulipwa Euro 600,000 kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Uganda (Cranes). Kaburu alisema kuwa wako katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho huo na wamefurahi kuona Okwi anapata timu Ulaya na kutimiza ndoto zake. Alisema pia Simba tayari imemsajili beki wa APR, Mbuyi Twite na atatua nchini wakati wowote kabla ya tamasha la Simba Day ambalo litafanyika Agosti 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Alieleza kuwa Simba imeingia mkataba wa miaka miwili na beki huyo ambaye anachukua nafasi ya Lino Masombo aliyeachwa baada ya kiwango chake kutoridhisha. Wakati huo huo, taarifa kutoka Simba zinaeleza kwamba wachezaji wake wengine chipukizi watano wa Simba B ambao walikwenda Ujerumani na timu yao ya kituo cha soka cha jijini Mwanza wamepata timu mbalimbali za kuchezea za Ujerumani na Austria. Habari zinaeleza kwamba wachezaji hao watarejea nchini na klabu hizo zitaanza taratibu za kuingia nao mikataba. Wachezaji hao yosso waliong'aa ni pamoja na kipa Aboubakar Hashim, Said Ndebla, Miraji Athumani, Frank Sekule (washambuliaji) na Hassan Hassan. Mwaka jana Simba ilimuuza mshambuliaji Mbwana Samatta kwa TP Mazembe kwa dola za Marekani 150,000 na baadaye Patrick Ochan. CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment