STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 25, 2012

Hassani Kumbi: Kiungo mkabaji anayetesa na miondoko ya Mduara

AWALI ndoto zake tangu akiwa shuleni ilikuwa kuja kuwa nyota wa soka akimudu nafasi ya kiungo mkabaji na nafasi nyingine za mbele akitamba na timu kadhaa ikiwemo Ajax Mzamba ya Temeke alioshiriki nao Ligi ya Taifa. Hata hivyo kitendo cha kupigwa bisibisi katika mechi ya 'mchangani' ya Ligi ya kuwania Ng'ombe, Kiwalani, lilisitisha ndoto za Hassani Kumbi ' H-Kumbi au 'H-Kilakitu' na kujikuta akihamia kwenye fani ya muziki. Kumbi, alisema baba yake alimpiga marufuku kucheza soka baada ya tukio hilo lilomfanya alazwe hospitalini na alipopona aliamua kuingia katika muziki kwa vile alishawahi kuimba kaswida alipokuwa madrasa. Msanii huyo anayetamba baada ya kuibuliwa na kituo cha Mkubwa na Wanae kinachoendeshwa na Said Fella, alisema alipigwa bisibisi hiyo mbavuni na mmoja wa mashabiki wa timu pinzani iliyocheza na timu yake ya Young Stars. "Baba alinizuia kucheza soka baada ya kitendo cha kujeruhiwa uwanjani ndipo nikahamishia makali yangu kwenye muziki baada ya kupita usaili wa Mkubwa na Wanae," alisema. Kumbi alisema baadhi ya nyota aliocheza nao shuleni na kwenye timu kadhaa ni Abuu Ubwa, Nizar Khalfan, Adam Kingwande, Ramadhani Chombo, Juma Jabu na Ally Mustafa 'Barthez'. Mkali huyo anayetamba kwa sasa na kibao cha 'Vocha' alichoimba na Dogo Aslay waliopo naye kituo cha Mkubwa na Wanae, alisema licha ya kuimba kaswida, pia aliwapenda mno Banzastone na Zahiri Ally Zorro. "Nilivutiwa na Banzastone na Zahir Ally ambao hata leo wanawafuatilia ndio maana nimeweza kuinuka haraka kisanii," alisema. Msanii huyo, anayetarajia kuachia kazi mpya iitwayo 'Sindano' akiwa na video yake huku akikamilisha pia kibao cha Deni alichoimba na AT, alisema muziki kwa sasa nchini unalipa na una mafanikio makubwa. Alisema zamani ilikuwa vigumu msanii wa muziki wa kizazi kipya kuandaa shoo ya kiingilio cha Sh 20,000 au 50,000 lakini sasa inawezekana akitolea mfano tukio la Diamond alipofanya onyesho lake la 'Diamond Are Forever'. Kumbi, anayetamani kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa mara 'kijiwe' cha muziki kitakampomchanganyia, alisema licha ya muziki kulipa bado vipo vikwazo ikiwemo uharamia na unyonyaji unaofanywa dhidi ya kazi za wasanii. Alisema ni vema serikali ikawasaidia wasanii kwa kutunga sheria kali ili kuwatia adabu wezi wa kazi za wasanii, sambamba na kuvuna mapato yaliyopo katika fani hiyo, akidai fedha nyingi zinapotea mikononi mwa 'wahuni'. Msanii huyo anayependa kula wali kwa maharage au ugali kwa samaki wa kukangaa na mlenda pamoja na kunywa juisi ya Embe, alisema kama angekutana na Rais angemweleza jambo hilo sambamba na kumsihi aboreshe maisha ya watanzania hasa huduma za kijamii na kudhibiti mfumuko mkubwa wa bei za vyakula na bidhaa nyingine. Kumbi anayeishabikia Simba na Manchester United na kuwazimia wachezaji nyota wa timu hizo, Haruna Moshi 'Boban' na Javier Hernandez 'Chicharito', alisema kati ya matukio ya furaha kwake ni kukubalika kwa kazi yake ya kwanza ya 'Vocha' na pia kukutana kwa mara ya kwanza na kuzungumza na Zahir Ally Zorro anayemhusudu na kumsifia uwezo alionao. "Nilisisimka mno nilipokutana uso kwa uso na Zahir Ally na kujisikia faraja aliponieleza kwamba naweza, pia nilipoachia kazi yangu ya Vocha na kupokelewa vema na kwa huzuni ni msiba wa baba yangu Ally Kumbi na kuuguliwa na mama yangu hadi leo," alisema Kumbi. Mkali huyo aliyeoana na Aisha Soud na kuzaa nae mtoto mmoja aitwae Hawa (2), alisema matarajio yake ni kuhakikisha anafika mbali katika muziki, pia akiweka wazi kwamba yeye ni H Kila Kitu akimaanisha anaimba miondoko yote ya muziki ikiwemo taarab na dansi. Kumbi anayemshukuru Mungu na watu waliomsaidia katika muziki kama Said Fella, Yusuf Chambuso, Suleiman Daud 'Sulesh' na wasanii wenzake wa Mkubwa na Wanae, alisema kitu cha thamani anachokumbuka kununua kwa fedha zake za muziki ni kumuugizia mwanae. "Nakumbuka nilienda kufanya shoo Iringa na kupata fedha nyingi kwa mara ya kwanza katika maisha yangu bya muziki na niliporejaea Dar nilikuwa mwanangu Hawa mgonjwa hivyo nikatumia kumtibia pamoja na kumnunulia nguo za bei mbaya," alisema. Msanii mwenye ndoto za kuja kujitolea kuwasaidia wengine kama anavyofanya Mkubwa Fella, alitoa ushauri kwa watu matajiri kuwasaidia wasanii kuwaibua na kuwaendeleza badala ya kusubiri watu wengine wawaibue kisha kuwarubuni wasanii hao bila kujua walikotokea. "Wapo watu wenye fedha zao wamekuwa wakifanya hila kuwarubuni wasanii chipukizi baada ya kuona wameanza kutoka kwa kuinuliwa na watu kama THT, Mkubwa na Wanae au Tip Top Connection, hii sio haki kwanini wasitumie fedha zao kufanya kama wenzao?" Alihoji. Hassani Ally Kumbi, alizaliwa Juni 16, 1987 akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto wanne na kusoma Shule ya Msingi Mabatini -Tandika Dar es Salaam kabla ya kuendelea na masomo ya Sekondari alipohitimu kidato cha nne mwaka 2006 Shule ya Twaybat pia ya Temeke. Alienda kusomea ufundi umeme wa magari mjini Morogoro kabla ya kuzama kwenye soka aliloanza kucheza tangu akisoma shule ya msingi, timu yake ya chandimu ikiwa ni Santiago Chile maarufu kama G Stiva akimudu namba 6 na nyingine zote za mbele. Timu nyingine alizozichezea kabla ya kutua kwenye muziki ni Good Hope, TMK Kids, DYOC na Ajax Mzamba aliyoitoa daraja la tatu hadi Ligi ya Taifa ya TFF. Mwisho

No comments:

Post a Comment