STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 1, 2014

Yanga yavunja mwiko Taifa, yaidonyoa Al Ahly 1-0, Gor Mahia yafa nyumbani KCCA yaambulia sare ugenini

Mshambuliaji wa Yanga Mrisho Ngassa akichuana na mchezaji wa Al Ahly katika mechi yao leo uwanja wa Taifa (Picha:Habari Mseto)
Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly waliokaa kwa Yanga 1-0 leo
Wanaumeeeeee! Yanga walioifumua Al Ahly na kuvunja mwiko wa unyonge kwa timu za Kiarabu Afrika
HATIMAYE mabingwa wa soka nchini, Yanga imekata mzizi wa fitina baada ya kuvunja mwiko kwa timu za Misri kwa kuwanyuka mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika , Al Ahly ya Misri wakielekea kufuata nyayo za watani za Simba walipointoa Zamalek mwaka 2003.
Bao pekee lililofungwa kwa kichwa dakika ya 82 na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' akiunganisha mpira wa kona iliyochegwa na Simon Msuva, ilitosha kuipa ushindi kiduchu Yanga na kuwa na jukumu la kulazimisha sare yoyote ugenini ili kufuzu hatua ya 16 Bora.
Hata hivyo Yanga hasa washambuliaji wao watajilaumu kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga ambazo zilipotezwa kwenye vipindi vyote viwili ambapo kama zingetumiwa vyema timu hiyo ingeweza kuibuka na ushindi mnono na kuiweka pagumu Al Ahly.
Washambuliaji Hamis Kiiza, Mrisho Ngassa na Emmanuel Okwi walikosa mabao zaidi ya matatu ya wazi kipindi cha pili kabla ya kipindi cha pili kuendelea hata walipoingizwa Didier Kavumbagu na Said Bahanuzi.
Yanga, ambayo ilikuwa haijawahi kuifunga timu yoyote ya Misri, imewapa burudani mashabiki waliofurika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao ulishuhudia kikundi cha mashabiki wanaohisiwa wa Simba kung'oa viti kabla na baada ya Yanga kupata bao.
Haikufahamika sababu za mashabiki hao kuamua kung'oa viti na kusababisha askari wa FFU kuwa na kazi nyingine ya kuwaonya, lakini kwa hakika ni uhuni usiokubalika kwa sababu uwanja wa Taifa umegharamiwa na haikupaswa mashabiki hao kufanya kitendo hicho katika mechi ya kimataifa inayohusisha watani zao.
Kwa matokeo hayo Yanga imevunja mwiko kwa timu za Misri ikiwemo hiyo Al Ahly, na kuwa na kazi ya kusaka sare ugenini ili kuweza kusonga mbele na kurudia historia iliyowekwa na Simba mwaka 2003 walipoivua taji Zamalek waliowala bao 1-0 jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa idadi kama hiyo ugenini na kushinda kwa mikwaju ya penati 3-2.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo, Gor Mahia ya Kenya imejikuta ikiloa nyumbani baada ya kulazwa mabao 3-2 na Esperance ya Tunisia, Dynamos ya Zambia ilitoka suluhu ya 0-0 na Vita Club ya DR Congo, nao mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, KCCA ya Uganda ilipata sare ya kuvutia ya mabao 2-2 dhidi ya wenyeji wao Nkana Red Devils ya Zambia.
No comments:

Post a Comment