STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 1, 2014

Yanga, Al Ahly hapatoshi leo, Jangwani waonywa

Yanga
WACHEZAJI wa klabu ya Yanga wametahadharishwa kucheza kwa umakini mkubwa na kushambulia kusaka mabao mapema katika mechi yao ya leo dhidi ya Al Ahly kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga wanavaana na mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika na washindi mara sita wa Super Cup kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo, huku ikiwa na rekodi mbaya dhidi ya timu za Waarabu, licha ya kuweka rekodi hivi karibuni ya kushinda jumla ya mabao 19 katika mechi zao tatu ilizocheza ndani ya wiki mbili.
Kwa kutambua ugumu wa mpambano huo, nyota wa zamani wa timu hiyo, Edibily Lunyamila na Ramadhani Kampira wamewauma sikio wachezaji wa Yanga kwa kuwataka kucheza 'jihad' na kwa umakini mkubwa ili wasiwape nafasi wageni wao kupata mabao au sare ya aina yoyote.
Kampira, alisema anaamini vijana wa Johannes van der Pluijm wakishambulia na kupata mabao mengi katika mechi ya leo, nafasi yao ya kuiondosha Al Ahly na kuweka rekodi mpya kwao Cairo ni nyepesi.
"Wito wangu kwa mabeki kucheza kwa umakini mkubwa ili kutoruhusu Al Ahly kupata bao lolote au kulazimisha sare, na safu ya ushambuliaji inaonekena kuelewana, ihakikishe inafunga mabao mengi ya kutosha ili yaisaidie timu kwa mechi ya marudiano ambayo naamini itakuwa ngumu kama desturi za timu za Misri zikiwa kwao," alisema Kampira.
Naye Lunyamila alisema Yanga haipaswi kuichukulia kiwepesi wapinzani wao na badala yake washuke uwanjani kutafuta ushindi mnono huku wajilinda lango lao lisiguswe.
"Yanga ni timu nzuri, ina wachezaji wenye vipaji na wanaojua soka, lakini bado ina kazi ngumu kwa Al Ahly, icheze kwa umakini mkubwa hasa safu ya nyuma na viungo kuwazuia Waarabu hao wasipate mabao na washambuliaji nao wazitumie nafasi watakazopata kufunga mabao mengi ya kutosha ili kujiweka nafasi nzuri kwa mechi ya marudiano ugenini," alinukuliwa Lunyamila.
Lunyamila, winga nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema wachezaji wasibweteke na kauli za kutiana moyo kwamba watetezi hao kwa sasa wamechoka kwani jambo hilo siyo la kweli na wenzao wana uzoefu mkubwa na pia wanajua kufanya hila kwa mechi za marudiano wakificha makucha katika mechi za ugenini.
Yanga ambayo tangu ianze kushiriki michuano ya kimataifa ya Afrika haijawahi kuitoa timu yoyote ya 'Kiarabu' ilifika hatua hiyo baada ya kuitoa Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2 baada ya awali kuilaza mabao 7-0 na kwenda kuifunga kwao 5-2 na wiki iliyopita ilipata ushindi wa kishindo katika Ligi Kuu kwa kuicharaza Ruvu Shooting mabao 7-0.

No comments:

Post a Comment