STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, July 25, 2013

Msondo yaingia studio, kula Idd Dar, Zenji

Baadhi ya wanamuziki wa Msondo Ngoma wakiwajibika
BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' imetumia muda wake wa mapumziko kuingia studio kurekodi nyimbo zilizosalia za albamu yao, huku ikiweka bayana ratiba nzima ya Sikukuu za Idd el Fitri.
Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila 'Super D' aliiambia MICHARAZO kuwa, wameona ni vyema kuutupia muda wa likizo ya mfungo wa Ramadhani kurekodi nyimbo za albamu yao ambayo inasubiriwa kwa muda mrefu na mashabiki wao.
Super D, alisema nyimbo zinazorekodiwa kwa sasa katika studio moja ya jijini Dar es Salaam ni Lipi Jema na Baba Kibebe zilizotungwa na Eddo Sanga, Kwa Mjomba Hakuna Urithi wa Huruka Uvuruge, Nadhiri ya Mapenzi wa Juma Katundu na Machimbo.
Wimbo wa Machimbo umeingia kwenye albamu hiyo baada ya kuondolewa kwa kibao kilichokuwa kimetungwa na aliyekuwa muimbaji wao, Isihaka Katima 'Papa Upanga' uitwao 'Dawa ya Deni' na kibao cha mwisho cha albamu hiyo kilichobeba jina wa Suluhu wenyewe ulishakamilika kitambo.
Aidha Super D aliweka wazi kwamba bendi yao katika shamrashamra za Sikukuu za Idd el Fitri, watatambulisha baadhi ya nyimbo mpya katika maonyesho yatakayofanyika kwenye ukumbi wa  DDC Kariakoo kwa onyesho la Idd Mosi na Idd Pili watakamua TCC Chang'ombe kabla ya kuvuka bahari kuelekea Zanzibar kwa onyesho la Idd Tatu pale Gymkhan.
"Idd Mosi tutakamua ngome ya zamani ya wapinzani wetu, DDC Kariakoo na siku inayofuata tutaila Idd viwanja vya TCC Chang'ombe kisha kwenda Zanzibar kumalizia sikukuu," alisema Super.

No comments:

Post a Comment