STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 12, 2013

Kigogo Yanga matatani, kisa...!

Makamui Mwenyekiti wa Yanga, Clement  Sanga
MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga, anatarajiwa kufikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu kufuatia kauli aliyoitoa hivi karibuni kuwa timu yao inayoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwamba inahujumiwa na ndiyo maana mechi yao dhidi ya JKT Oljoro imesogezwa mbele na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Awali, mechi hiyo ya Yanga dhidi ya Oljoro ilipangwa kufanyika juzi (Jumatano ya Aprili 10) lakini sasa itachezwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa kauli kama za Sanga zinachangia kujenga chuki  zisizokuwa na sababu kati ya shirikisho hilo na mashabiki wa soka nchini.
Kwa sababu hiyo, Osiah alisema kuwa Sanga atatakiwa athibitishe ni kwa namna gani Yanga inahujumiwa baada ya kuwapo kwa mabadiliko hayo ya ratiba ambayo yalizihusu pia timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, zikiwamo za Simba na Azam ambazo sasa zitacheza Jumapili.
Osiah alisema kuwa anashangaa kusikia madai ya Sanga kuwa klabu hazijashirikishwa katika kufanya marekebisho hayo wakati ukweli ni kwamba klabu hizo ziliwakilishwa na viongozi wao walioko kwenye kamati ya ligi na timu yao ina mjumbe kwenye kamati hiyo.
Katibu huyo wa TFF alisema kuwa viongozi wa klabu walielezwa katika kikao kilichofanyika mapema kabla ya ligi kuanza kwamba kutakuwa na 'Super Week' katika hatua ya mwisho wa ligi ambayo itatekelezwa kupitia nafasi itakayopatikana katika kituo cha televisheni ya kulipia cha Afrika Kusini cha  Super Sport.
"Mnapotafuta wadhamini kuna wakati ni lazima mjitoe mhanga... na kuonekana kwetu kupitia Super Sport kumesaidia kuleta wadhamini wengi ambao tayari wamevutiwa na ligi yetu," alisema Osiah.
Katika mahojiano yake na vyombo vya habari hivi karibuni, Sanga alisema kuwa wao walikuwa tayari wameshaiandaa timu yao na kwa mabadiliko hayo ambayo hawaoni faida yake zaidi ya kuwapunguzia mashabiki viwanjani yamewapa hasara kubwa itokanayo na kuendelea kuiweka timu kambini.
Aliyewahi kuwa Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage waliwahi kuadhibiwa na TFF baada ya kukutwa na hatia ya kutoa kauli ambazo baadaye walishindwa kuzithibitisha.


Chanzo:NIPASHE

No comments:

Post a Comment