STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 12, 2013

UJUMBE WA FIFA KUWASILI APRILI 15




Na Boniface Wambura
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kuwatangazia wadau wa mpira wa miguu kuwa ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utawasili nchini Jumatatu (Aprili 15 mwaka huu) kwa ajili ya kushughulikia mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka FIFA, ujumbe huo utaongozwa na Mkuu wa Idara ya Uanachama ya FIFA, Primo Covarro na utafanya kazi kwa siku tatu kuanzia siku ya ujio na kuondoka Aprili 18 mwaka huu.

Ukiwa nchini, ujumbe huo utakutana na wagombea uongozi walioathiriwa na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambao waliomba mashauri yao yaangaliwe upya, wagombea ambao walikata rufani FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Rufani na Sekretarieti ya TFF.

Wajumbe hao wangependa kukutana na waziri anayehusika na michezo, hivyo TFF imeiandikia Wizara ikipendekeza kuwa ujumbe huo ukutane na Waziri na wakuu wengine wa michezo Aprili 16 mwaka huu 2013 kabla ya kuanza kazi zao.

Wagombea watakaosikilizwa na ujumbe huo wa FIFA ni:
1.   Farid Salim Mbaraka Nahdi: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi na baadaye rufani yake kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kutupwa na hali kadhalika ombi lake la kutaka shauri lake liangaliwe upya, kukataliwa.

2.   Elliud Peter Mvella: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kukata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kabla ya maombi yake ya kutaka shauri lake kuangaliwa upya, kukataliwa.


3.   Mbasha Matutu: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi na kukata rufani ambayo pia ilitupwa kabla ya kuomba shauri lake liangaliwe upya, ombi ambalo lilikataliwa.

4.   Hamad Yahya: Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na kuondolewa. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ikatupa ombi lake.

5.   Jamal Emily Malinzi: Mgombea wa nafasi ya urais wa TFF ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, hivyo kuondolewa kwenye mchakato. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini likakataliwa. Hata hivyo, alikuwa ameshakata rufani FIFA.

6.   Michael Wambura: Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na rufani yake kukataliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF. Hakuomba shauri lake liangaliwe upya, lakini alikata rufani FIFA.

Shirikisho linawaomba wote waliotajwa hapo juu kujiandaa kwa utetezi na maelezo ya kutosha na kwamba barua za kuwaita zinafuata. (Orodha ya waathiriwa na programu ya ujumbe wa FIFA imeambatanishwa)

No comments:

Post a Comment