STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 22, 2012

Sita Simba hatarini kupigwa panga

HATMA ya wachezaji sita wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam, iko shakani baada ya mikataba ya kuichezea klabu hiyo kumalizika huku kikao cha Kamati ya Usajili kilichofanyika juzi usiku kikishindwa kufikia maamuzi ya kuwapa mikataba mipya. Nyota hao ambao kanuni zinawaruhusu kufanya mazungumzo na klabu yoyote sasa ni pamoja na Ally Mustapha 'Barthez', Uhuru Suleiman, Juma Jabu, Juma Nyosso, Derick Walulya na Gervais Kago, ambaye ni kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati. Uhuru alithibisha kuwa hana mkataba na Simba hivi sasa na yoyote anayemuhitaji milango iko wazi kumfuata. "Ila Simba ni zaidi, wamenisaidia sana (wakati alipovunjika mguu) siwezi kuwasahau," alisema kiungo huyo. Hata hivyo, wachezaji Mganda Walulya na Kago tayari wameshatupiwa virago na msimu ujao hawatavaa jezi tena za klabu hiyo, habari hizo zilisema. "Kago si mbaya ila ameshindwa kuendana na mfumo unaotumika sasa katika timu yetu ila bado timu yake ya taifa (Jamhuri ya Afrika ya Kati) inamuhitaji, Walulya amekuwa mzito na anashindwa kumudu kasi ya washambuliaji anaowakaba," alisema mmoja wa viongozi wa kamati ya usajili. Kiongozi huyo alisema kuwa kamati inaendelea kufanyia kazi ushauri kutoka katika benchi la ufundi la timu hiyo ili kuziba nafasi zenye mapungufu na hatimaye kufanya vizuri kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yanayotarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia mwezi ujao. Aliwataja wachezaji wapya waliosajiliwa kuwa ni mshambuliaji Abdallah Juma kutoka JKT Ruvu, kiungo mmoja wa DC Motema Pembe huku pia Simba ikipanga kwenda Uganda kumfuata Mussa Mude ambaye pia anawaniwa na Azam na Santos ya Afrika Kusini. Kamati ya Usajili ya Simba inaongozwa na mwenyekiti wake, Hanspope Zacharia, ambaye Ijumaa iliyopita alitarajia kumsainisha marehemu Patrick Mafisango, lakini mipango hiyo haikutimia kufuatia ajali iliyotokea asubuhi ya siku hiyo na kuchukua uhai wa kiungo huyo mkabaji aliyekuwa na uraia wa Rwanda. Wachezaji nyota wengine waliobaki akiwemo Juma Kaseja, Emmanuel Okwi, Mwinyi Kazimoto, Shomary Kapombe, Kevin Yondani, Haruna Moshi 'Boban', Salum Machaku, Felix Sunzu, Nassor Masoud 'Chollo', Amir Maftah na yosso kutoka Simba B waliopandishwa wote mikataba yao bado haijaisha. Chanzo;NIPASHE

No comments:

Post a Comment