STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 22, 2012

Doyi Moke: Kipa wa zamani aliyejitosa kwenye biashara ya madini

TANGU alipostaafu baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa, kipa wa zamani wa timu za Majimaji ya Songea, Simba na Yanga, Doyi Moke, amewekeza nguvu zake katika biashara za kununua na kuuza madini katika nchi za Afrika. Nyota huyo aliyeibebesha taji la ubingwa wa Ligi ya Muungano, Majimaji mwaka 1997, alisema amejikita katika shughuli hiyo kwa fedha za soka. Alisema japo soka halikumpa fedha nyingi, lakini kidogo alichopata aliweka akiba inayomfanya leo aishi maisha mazuri akifanya biashara hiyo ya madini akishirikiana na nduguze. Moke, mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliyeanza kucheza soka tangu Shule ya Msingi na kucheza soka la kulipwa akiwa na miaka 17 tu katika timu ya Muungano ya Bukavu, anauza madini chini ya kampuni yake. Kampuni hiyo inaitwa GFK Limited, yeye akiwa ndiye Mkurugenzi akinunua madini kama almasi na dhahabu toka Kongo na kuuza Tanzania na nchi nyingine za Afrika na kumfanya awe mtu wa kusafiri. Moke alisema kabla ya kufanya biashara hiyo alijikita katika biashara nyingine mara alipotundika daluga mwaka 2003 hata hivyo hazikumlipa kama biashara yake ya sasa. Mkali huyo aliyewahi kuwika pia na timu za Aspwara, Rayon za Rwanda na Afya Sport ya Goma, alisema ni vema wachezaji wa sasa wakawa makini na kile wanazovuna katika soka kwa ajili ya manufaa ya ya baadae. "Tulipokuwa tukicheza fedha hazikuwepo kama leo, hata hivyo baadhi yetu tulikuwa na fikra za mbali ndio maana leo tunaishi vema, kwa wanaocheza sasa ni wajibu wao kukumbuka kesho yao kwa kujiwekea akiba," alisema. ALIPOTOKA Doyi Moke alizaliwa Oktoba 4, 1967 Bukavu nchini Zaire, sasa Kongo akiwa ni mtoto wa sita kati ya 10 wa familia yao. Shule ya Msingi aliisoma College Alfajiri kisha Atenend Banda Sec kabla ya kusomea Diploma ya Lugha ya Kifaransa. Kisoka alianza kucheza tangu kinda akidakia timu za shule na kutwaa nao mataji ya mashindano ya shule nchini mwao, akimtaja kocha Gabie Mugimbi kuwa ndiye aliyekivumbua kipaji chake. Moke alikiri alimvutiwa kisoka na nyota wa zamani wa Ufaransa Michel Platin na kuitaja klabu yake ya kwanza ya kulipwa kuwa ni Muungano aliotwaa nao taji la Ligi ya Mkoa wa Bukavu mwaka 1987. Baada ya kung'ara na timu hiyo kocha wa zamani wa Yanga, Raoul Shungu alimuona na kumpeleka Rwanda kuichezea ASPWARA 1989 kabla ya kutua Rayon Sport kwa muda na kurudi Kongo kuichezea Afya ya Goma. Alitua baadae Vital'O ya Burundi na kufanya mambo makubwa akiwapiku makipa wanne aliowakuta kikosi ikiwemo mmoja, Ramadhani Ally aliyemsusia jezi alipopewa nafasi mara ya kwanza kikosini. Alisema anakumbuka kocha alimpa nafasi katika mechi dhidi ya wapinzani wao Port Louis walioifunga mabao 2-0 na kujihakikishia namba akiipa ubingwa na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika 1992. Alisema aliachana na Vital'O mwaka 1995 aliposhuhudia mchezaji mwenzake, Kamala Jeff akipigwa risasi na waasi wa Burundi mpakani mwa nchi hiyo na Kongo na kuamua kuachana na soka ili aende Afrika Kusini kusaka maisha. "Hata hivyo nilipofika Tanzania nikielekea 'Bondeni', nilikutana Mackenzie Ramadhani aliyenishawishi kuendelea na soka na kunikutanisha na kocha Nzoysaba Tauzany, aliyenisajili kuichezea timu yake ya Majimaji," alisema. Alisema hakuamini alipopokelewa kama 'Mfalme' mjini Songea na viongozi wa mkoa akiwemo RC, ambaye kwa sasa ni Spika wa Bunge, Anne Makinda akitaja dau alilosajiliwa likiwa Sh 700,000. Baada ya kuipa ubingwa wa Muungano kutokana na kumaliza Ligi ya Tanzania Bara wakiwa watatu nyuma ya Yanga na Simba, mwaka 1999 alihama na kutua Simba alioichezea kwa mafanikio kabla ya kusajiliwa Yanga. Alisema aliamua kuachana na Simba baada ya 'kuzikwa' fedha zake za usajili na mmoja wa viongozi (jina kapuni) na kuhamia Yanga mwishoni mwa mwaka 2000 na kuichezea hadi mwaka 2003 alipoenda Rayon Sport na kustaafu huko. Alisema tangu alipostaafu amekuwa mshauri kwa klabu ya Yanga na wachezaji wanaocheza sasa, pia akimpiga tafu shemejie, Henry Kalekwa anayemiliki timu ya Sofapaka ya Kenya. Moke anayependa kula wali kwa kisamvu na kunywa bia ya Safari, alisema kati ya klabu zote alizochezea, Vital'O na Yanga ndizo bomba kwake. Alisema mbali na kuichezea, pia yeye ni mshabiki mkubwa wa Yanga, Arsenal na TP Mazembe, huku akidai anapenda kuogelea na kubadilishana mawazo. HUJUMA Moke aliyemtaja Mbwana Samatta anayecheza TP Mazembe kama 'nembo' ya Tanzania katika soka la kulipwa kwa kipaji kikubwa alichonacho, alisema ndani ya soka amekumbana na mambo mengi. Alitaja mojawapo ni tuhuma alizodai kubambikiwa klabu ya Simba akidaiwa kuihujumu timu hiyo dhidi ya Yanga katika mechi iliyochezwa mwaka 2000 ambapo Yanga walishinda 2-0 kwa mabao ya 'Bwana Harusi' Idd Moshi. "Jambo hilo linaniuma hadi sasa na ndilo lililonifanya niichukie Simba kwa vile uongozi uliamua kunipakazia baada ya kuumbua kwa wanahabari juu ya kunizika fedha zangu za usajili," alisema. Juu ya mechi ngumu, Moke, alisema ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001 akiichezea Yanga na Highlander ya Zimbabwe lililochezwa Harare ambapo Yanga ilishakata tamaa baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani. "Naikumbuka kwa namna nilivyowaapia wanayanga waliokata tamaa na kutishwa na kauli ya kocha wa Highlander aliyetutaka tusisumbuke kuwafuata kwao kwa maana tulikuwa tunajisumbua tu," alisema. Alisema hata hivyo aliwapa moyo wenzake na kwenda kufanya vitu adiumu uwanjani na kuisaidia Yanga kushinda mabao 2-0 na kusonga mbele. Moke aliyemhofia Mohammed Husseni 'Mmachinga', alisema soka la Bongo, litasonga mbele iwapo nyota wa zamani watapewa nafasi za kuongoza klabu na FA badala ya 'wavamizi' wanaotambia elimu zao kubwa. Alisema wengi wa viongozi waliojipenyeza kwenye soka wanafanya hivyo kwa kusaka masilahi ikiwemo umaarufu wa kugombea nafasi za kisiasa, huku wakiliacha soka likiporomoka. "Ni kweli elimu ni kitu cha muhimu, ila wachezaji wa zamani wana umuhimu katika kuinua soka la Tanzania, watumiwe kama wenzetu wanavyowatumia wachezaji wao," alisema. Moke anayesikitishwa na kifo cha baba yake kilichotokea akiwa na miaka 13 tu, ameoa na ana watoto wawili, pia aliwashukuru mama yake mzazi kwa jinsi alivyomlea na kumuongoza hadi kufika alipo, sambamba na Rashid Haradee na marehemu Tauzany. Aliwaasa wachezaji kujituma na kutambua soka ni ajira lao, sambamba na kuzipigania klabu na timu za taifa pale wanapozichezea ili kuzisaidia na kujitangaza vema kimataifa. --------------------

No comments:

Post a Comment