STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 22, 2012

Ramadhani Singano: Messi wa Simba anayemzimia Boban

<
KIPAJI kikubwa cha soka alichonacho hasa kumiliki mpira, kupiga chenga, mbio na kufunga, kimemfanya kinda la timu ya Simba, Ramadhani Singano kufananishwa na nyota wa Barcelona, Lionel Messi. Wadau wa soka hasa wa klabu ya Simba humfahamu zaidi kwa jina la Messi kuliko majina yake halisi, wakimlinganisha kiuchezaji na nyota huyo wa Argentina anayetajwa kama mwenye kipaji cha pekee duniani. Licha ya kufurahia jina hilo, Singano anakiri hajafikia hata robo ya umahiri wa Messi anayemhusudu na kumuiga uchezaji wake. Singano, aliyewapoteza wazazi wake akiwa na miaka 11, alisema anamshukuru Mungu kwa kumjalia kipaji hicho, ila anaamini ana kazi kubwa ya kufika alipo 'wajina' wake. Hata hivyo, Messi aliyeanza kucheza kama beki enzi za soka la chandimu, alisema nidhamu, mazoezi, kujituma na kumtumainia Mungu kutamfikisha mbali kisoka. "Naamini nikijituma zaidi, nikazingatia nidhamu na kumtanguliza Allah, katika kila kitu, nitafika mbali kwani najiamini naweza," alisema. Messi, alizichezea timu za Ubatani na Bombom kabla ya kuonwa na Simba B, alisema japo hana muda mrefu katika soka, anashukuru mafanikio aliyopata. "Soka limenisaidia mengi kimaisha na kiuchumi, ila sipendi yaandikwe, lakini kufahamika, kuheshimiwa na kumudu kuwasaidia ndugu na jamaa zangu, ni vitu vya kujivunia," alisema. Pia, alisema kutwaa mataji, medali na tuzo mbalimbali akiwa na Bombom na Simba B, ikiwemo kuwa Mchezaji Bora mara tatu katika michuano ya Rolling Stone, Uhai Cup na Copa Coca Cola 2009 ni mengine yanayomfariji. "Mwaka jana pekee nimetwaa mataji mawili ya Uhai na Kinesi nikiwa Simba B na msimu huu nimesherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara nikiwa na Simba," alisema. Messi, anayemzimia na kuvutiwa na soka la Haruna Moshi 'Boban', alisema hakuna tukio la furaha kwake kama alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mchezaji bora wa michuano ya Uhai-2009. "Furaha niliyokuwa nayo ilinifanya nigawe fedha za zawadi kwa wachezaji wenzangu wa Simba B, nakumbuka nilitoa Sh. 150,000 kati ya 400,000," alisema. Kwa matukio ya huzuni, Messi alisema ni kuwapoteza wazazi akiwa mdogo na kunusurika kufa kwa ajali ya gari alipotoka kumzika baba yake mjini Tanga mwaka 2003. Mchezaji huyo anayependa kula mihogo ya kuchemsha, ugali kwa bamia na kunywa juisi ya Parachichi, alisema hupenda kutumia muda wake mwingi kufanya ibada na kuangalia 'muvi' hasa za filamu za Jean Claud van Damme. Aliwashukuru makocha wake, Ahmed Mohammed Kibonge, Teddy na Bosco waliokivumbua na kukiendeleza kipaji chake kiasi cha leo kuonekana 'lulu'. "Nawashukuru mno hasa Kibonge aliyetambua kipaji changu wakati anasoma Shule ya Sekondari Al Farouk na kunipeleka katika timu yake ya Bombom." Alisema, Simba B ilivutiwa naye baada ya kung'ara katika mechi dhidi ya Bombom na kusajiliwa katika kikosi hicho mwaka 2009 na kuja kupandishwa timu ya wakubwa msimu huu akiwa na wenzake wanne. Messi, anayemudu karibu nafasi zote dimbani, japo hufarahia kucheza kama mshambuliaji, alisema hawezi kuzisahau mechi mbili akiwa na Simba dhidi ya Azam na Kiyovu Sport ya Rwanda katika Kombe la Shirikisho Afrika. "Nazikumbuka kwa vile zilizokuwa mechi kubwa za kwanza kwangu na namna nilivyoonyesha kiwango cha hali ya juu nikisaidia moja ya mabao mawili ya ushindi dhidi ya Azam katika Ligi Kuu," alisema. Mkali huyo anayeota kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na kuanzisha asasi ya kusaidia yatima na wenye matatizo, alisema soka la Bongo lipo juu, ila baadhi ya wachezaji hawajitambui na kuchangia kulikwamisha. Alisema huenda kukosa misingi bora ya soka ni tatizo kwa wachezaji nchini, ila aliwataka wazinduke na kutambua soka ni ajira yao hivyo walitumikie kwa ufanisi ili wafike mbali kama nyota wa mataifa mengine ni tatizo. Pia, alidai tabia ya wadau kuwaingilia kazi makocha na kuwakatisha tamaa wachezaji ni tatizo jingine, sawa na kukosekana kwa wadhamini katika soka la vijana. Alisema angekutana na Rais, licha ya kumuomba aboreshe miundo mbinu na huduma za jamii, angemsihi pia atumie nafasi yake kushawishi wawekezaji na wafadhili kuangalia soka la vijana na timu nyingine ndogondogo. Ila yeye angelikuwa ni Rais, angeboresha huduma za jamii hasa elimu na kuwekeza katika michezo akidai ni njia nzuri ya kusaidia ajira kwa wengi. Kuhusu Stars, alisema timu hiyo inashindwa kufanya vema kutokana na tabia ya u-Simba na u-Yanga inayoendekezwa na wadau wakiwemo hata wachezaji, pia kuingiliwa kazi kwa makocha wa timu hiyo. "Tunaweza kufuzu fainali za Afrika na Dunia, kama wadau wataacha u-simba na u-yanga unaowaathiri hata wachezaji, pia makocha waachiwe wafanye kazi na timu ziandaliwe vema," alisema. Shabiki huyo wa Manchester United anayechizishwa na nguo za rangi yoyote, alisema anaamini kila mmoja akitimiza wajibu wake katika klabu au timu ya taifa, Tanzania zitaweza kutamba kimataifa. Ramadhani Yahya Singano, alizaliwa Desemba 31, 1992 akiwa ni mtoto wa mwisho wa familia ya watoto sita wa Yahya Singano mwenyeji wa Tanga akitanguliwa na kaka wanne na dada mmoja. Shule ya Msingi alisoma Mgulani kati ya mwaka 2000-2006 kabla ya kusoma kama yatima katika Shule ya Sekondari Al Farouk alipozidi kung'ara katika soka baada ya awali kuanza kucheza akiwa darasa la nne. Chandimu alilichezea timu ya G Spar Kavela, kabla ya kutua Ubatani akicheza nao michuano ya mchangani kisha kusajiliwa Bombom na baade Simba B. Kwa upande wa timu za taifa, alianza kuchezea timu za vijana U17 na U20 tangu 2010 kabla ya wiki iliyopita kuitwa Taifa Staras na kocha Kim Poulsen. --------------------

1 comment:

  1. Namfahamu, Alikuwa ni classmate wangu pale ALFARUK - TABATA..
    Kipaji chake aisee... hakuna maneno yatakayotosha kukielezea!

    Mimi ni shuhuda mzuri wa Hayo mliyoandika! NASEMA WAZI KWAMBA, RAMA ATAFIKA MBALI SANA..Coz anamtegemea Allah ktk kila jambo!

    viva singano...

    By Kishubiiiiiiiiiiiiiiii

    ReplyDelete