STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, April 7, 2014

Hatma Chelsea, Dortmund kufanya majabu gani Ulaya kesho?

HATMA ya vijana wa kocha Jose Mourinho, Chelsea ya Uingereza kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itajulikana kesho watakaporudiana na PSG ya Ufaransa kwenye uwanja wa Stanford Bridge jijini London baada ya kufungwa bao 3-1 ugenini Paris, Ufaransa.
Chelsea iliyo katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England, ina nafasi kubwa kupenya hatua hiyo kutokana na bao la ugenini ililopata, ambalo linaifanya kuhitaji bao 2-0 kutangulia hatua hiyo.
Hata hivyo, itakuwa na kibarua kigumu mbele ya matajiri wa Ufaransa ambao wangependa kutinga hatua hiyo baada  ya kipindi kirefu kupita bila kufikia nusu fainali licha ya kutumia fedha nyingi kujenga kikosi imara Ulaya.
Timu nne zitakazofuzu  nusu fainali zinatarajiwa kujulikana wiki hii wakati timu nane za robo fainali zitakapokuwa zikimalizia mechi zao za mkondo wa pili kati ya kesho na keshokutwa.
Ikiwa bila mfumania nyavu wake mahiri, Zlatan Ibrahimovic aliyeumia mechi iliyopita, PSG itawategemea wakali wengine akiwemo Ezequiel Lavezzi, Edinson Cavani ili kuipa wakati mgumu Chelsea na kutokubali kuwa daraja la kuwavusha wapinzani wao kuingia nusu fainali.
Kivumbi kingine cha mechi ya marudiano ya robo fainali kitakuwa nchini Ujerumani wakati Borussia Dortmund ikiwaalika Real Madrid wakiwa na machungu ya kubutuliwa bao 3-0 wiki iliyopita.
Real itahitaji sare ya aina yoyote ili kulipa kisasi kwa wapinzani wao waliowang'oa hatua ya nusu fainali mwaka jana kwa kipigo cha mabao 5-3, ilifungwa ugenini mabao 4-1 na kushinda nyumbani kwao 2-0 na kuiacha Dortmund ikienda kucheza fainali na Bayern.
Pamoja na kufungwa mabao 3-0 ugenini, Dortmund siyo timu ya kubezwa na huenda ikafanya maajabu kwa kuing'oa Real kwani itakuwa na 'muuaji' wake Robert Lewandowski aliyekuwa akitumikia kadi, licha ya kwamba kocha wa Real, Carlo Ancelotte ametamba wana kiu ya kutaka kunyakua ubingwa wa michuano hiyo mwaka huu.
Ancelotte alinukuliwa mbali na taji hilo pia anataka kunyakua mataji mengine mawili nyumbani kwao yaani Ligi Kuu wanaochuana na majirani zao Atletico Madrid na mahasimu wao Barcelona ambao wanakuna nao kwenye fainali ya Kombe la FA, taji jingine wanaloliwinda vijana hao wa Santiago Bernabeu.
Kivumbi cha ligi hiyo ya Ulaya kitaendelea Jumatano wakati, watetezi wa taji hilo, Bayern Munich watakapowakaribisha Mashetani Wekundu kwenye uwanja wao wa Allianz Arena. Mechi ya awali Munich ilifungana bao 1-1 na Manchester United.
Nazo timu zinazochuana kileleni mwa msimamo wa La Liga, Atletico Madrid na Barcelona zenyewe zitakuwa katika kitatange kingine mjini Madrid baada ya wiki iliyopita kushindwa kupata mbabe kati yao kwa sare ya bao 1-1.

No comments:

Post a Comment