Hassan Vocha, mmoja waimbaji wa Dar Modern Tarab |
Sikudhani Ally, muimbaji mwingine wa kundi la Dar Modern |
Akizungumza na MICHARAZO, mkurugenzi wa kundi hilo Hassan Bakar alisema kuwa video ya albamu hiyo itaingizwa sokoni kuanzia leo, huku ile nyingine ya 'Ooh My Honey' wakiiweka kiporo kwanza kwa kuhofia kuwakanganya mashabiki wao kama wangetoa video za albamu hizo mbili kwa mpigo.
Bakar alisema tayari baadhi ya video vya albamu hiyo zimeshaanza kurushwa hewani ili kuwaonyesha mashabiki uhondo uliopo katika albamu hiyo yenye nyimbo sita na nyimbo zake kuimbwa na nyota wao, Hassani Vocha, Mwanahawa Ally, Sikudhani Ally na wengine wanaounda kundi hilo lililorejea upya baada ya ukimya mrefu.
"Video ya albamu yetu ya 'Ngoma Imepasuka' itaachiwa Jumatatu, ingawa baadhi ya nyimbo tumeshasambaza na kurushwa na vituo vya runinga na sasa tunajipanga kwa ajili ya kuanza maonyesho ya mikoani kuzitangaza albamu hizo," alisema.
Bakar alisema wakati video yao ya albamu yao ya kwanza ikitoka pia kundi hilo lipo kwenye maandalizi makali kwa ajili ya onyesho maalum la 'Usiku wa Mwambao Asilia' ambalo watajumuika pamoja kutoa burudani na kundi la Naddi Ikhwan Safaa (Malindi).
"Tupo kwenye mandalizi makali ya onyesho hilo la Usiku wa Mwambao Asilia dhidi yetu na Malindi, ambapo mashabiki watapata kushuhudia taarab asilia ilivyo sambamba na kuwashuhudia magwiji wa miondoko hiyo kama Mohammed Elias," alisema Bakar.
Onyesho hilo litafanyika Aprili 19 kwenye ukumbi maarufu uliopo Magomeni, ambapo Dar Modern na Malindi watapiga nyimbo zao za zamani na mpya.
No comments:
Post a Comment