STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 12, 2011

Riyama Ally: Kisura mkali anayewagusa wengi







AKIIGIZA mwenye majonzi utamuonea huruma kwa jinsi atakavyolia kwa kumwaga machozi kama yupo msibani, akicheza kama mwendawazimu utamsikitikia kwa jinsi atakavyokuwa akila jalalani na kufanya vituko vyote wafanyavyo watu wenye kuugua kichaa.
Wengi hudhani yale anayoyafanya kwenye filamu ni mambo ya kweli kutokana na kucheza uhalisia asilimia 100, kitu kinachomfanya Riyama Ally kuwa mvuto wa pekee katika filamu anazoziigiza.
Mwanadada huyo mmoja wa waigizaji wa kike wakali nchini,alianza kufahamika mwishoni mwa miaka ya 1990 alipokuwa na kundi la Taswira na hasa igizo la Jabari lililokuwa likionyeshwa kwenye kituo cha ITV mwaka 2000.Katika igizo hilo lililokuwa gumzo nchini miaka hiyo, Riyama aliigiza kama mtoto aliyegeuzwa kichaa na mama yake mzazi aliyekosea masharti ya dawa za mganga ili kumdhibiti mumewe, ndilo lilothibitisha kuwa kisura huyo ni mkali.
Miaka mitatu baadae, yaani mwaka 2003 Riyama aliachana na Taswira na kutua kundi la Tamba Art, lililowahi kutamba na filamu kama Nsyuka na kuzidi kuonyesha makali yake.
Akiwa na kundi hilo linalomilikiwa na mganga maarufu wa tiba asilia, Dk Maneno Tamba, Riyama, alishiriki filamu mbalimbali zilizozidi kumjengea jina kutokana na staili yake ya uigizaji kama anayefanya kweli.
Baadhi ya filamu alizofyatua akiwa na kundi hilo ni pamoja na 'Miwani ya Maisha', 'Mzee wa Busara', Fungu la Kukosa na nyinginezo kabla ya kupata bahati ya kushiriki kazi nyingine nje ya kundi hilo.
Filamu kama 'My Darling','Simu ya Kifo', 'Darkness Night', 'Mwana Pango', 'Kolelo','Segito', Fake Promise na nyinginezo ni baadhi ya kazi hizo za nje zilizompaisha mrembo huyo mwenye asili ya mkoa wa Tanga.
Akiwa mmoja wa waigizaji wa kike wanaojiheshimu akiwa hana kashfa yoyote kama mastaa wengine wa aina yake, Riyama mbali na uigizaji, pia ni mtunzi wa filamu na mtayarishaji moja ya kazi yake binafsi ikiwa ni Mwasu iliyofanya vema sokoni kwa kitambo kirefu.
Riyama, mshindi wa tuzo ya Uigizaji Bora ya Risasi 2005-2006, kwa sasa yupo mbioni kuibuka na filamu mpya ya Second Wife, aliyoigiza na Vincent Kigosi 'Ray', Aisha Bui, Colleta Raymond na wengine.
Filamu hiyo inatarajiwa kuachiwa hadharani keshokutwa, ambapo kama kawaida yake, Riyama 'chozi' linamtoka kutokana na kutendwa sivyo ndivyo na 'mumewe' ndani ya filamu hiyo.
Riyama anayependa kusafiri, kupika na kulala anapokuwa nje ya fani yake ya uigizaji, ni shabiki mkubwa wa muziki wa taarab, kundi la Mambo Jambo na pia kusoma vitabu mbalimbali.

Mwisho

2 comments:

  1. hey riyama am mishy from kenya you are my star i like everything about you

    ReplyDelete
  2. Asiyekukubali ana jicho la husda, akae mbali nawewe.

    ReplyDelete