STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, January 14, 2014

Abdi Kassim aanza mambo Malaysia, mechi 4 bao 3

 KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa nchini Malaysia, Abdi Kassim 'Babi' ameanza makeke yake baada ya kuifungia timu yake mabao matatu katika mechi nne za kujipima nguvu alizocheza mpaka sasa wakijiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Babi alisajiliwa mwishoni mwa mwaka jana na klabu ya UiTM inayoshiriki ligi ya nchi hiyo na kwa sasa wanajifua tayari kwa msimu mpya utakaoanza Januari 21 badala ya Januari 18 kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Akizungumza na MICHARAZO toka Malaysia, Babi, alisema tangu ajiunge na timu hiyo wamecheza mechi nne za kujipima nguvu na yeye kufanikiwa kufunga mabao matatu, mawili katia mechi moja na jingine alifunga juzi wakati wakiizamisha San Dab Fc kwa bao 1-0.
"Kaka tupo kwenye maandalizi na tayari tumeshacheza mechi nne, tukishinda tatu na kupoteza moja, ambapo katika mechi hizo nimetupia mabao matatu, mawili kwenye mechi moja tuliyoshinda mabao 2-0 na nyingine ni leo (juzi) dhidi ya Sam Dab Fc nikifunga bao pekee," alisema Babi anayefahamika pia kama Ballack wa Unguja.
Alisema mechi yao ya kwanza kwa kupigwa mabao 3-1 kabla ya kushinda magoli 2-0 kisha kushinda  mechi mbili mfululizo kwa bao 1-0 na wanatarajia kucheza mechi nyingine kabla ya kusubiri kipute cha Ligi Kuu.
Babi aliingia mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea timu hiyo iliyomaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya tisa kati ya timu 12 baada ya kuichezea kwa kipindi kifupi KMKM ya Zanzibar iliyomsajili akitokea kuachana na Azam ya Tanzania Bara.
Kabla ya kuichezea Azam, Babi alikuwa akicheza soka la kulipwa katika klabu ya DT Long ya Vietnam akitokea Yanga aliyoichezea kwa mafanikio baada ya kung'ara akiwa na Mtibwa Sugar.

No comments:

Post a Comment