STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, May 28, 2012

Mpeni muda Kim atufikishe mbali kimataifa-Manyika

NYOTA wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuzichezea timu za Mtibwa, Sigara na Yanga, Manyika Peter, amewataka wadau wa soka nchini kumpa muda kocha Kim Poulsen, ili afanye kazi zake kwa manufaa ya soka la Tanzania. Pia, aliwataka wadau hao kutoweka matumaini makubwa ya timu yao ya taifa, Taifa Stars kufuzu fainali za Afrika 2013 au Kombe la Dunia 2014, ila nguvu ziwekezwe kwa fainali za mbele zaidi akiamini timu itakuwa imewiva. Manyika, alisema Tanzania imekuwa ikikwama kufika mbali kwa vile makocha wanaozifundisha timu za taifa na hata klabu hawapewi muda mrefu wa kukaa na timu husika, kitu alichotaka kisitokee tena kwa kocha wa sasa wa Stars. "Tumpeni nafasi Kim aweze kufanya kazi zake na naamini kwa uwezo alionao tunaweza kufika mbali zaidi na hapa tulipo, ila kama tutaendelea na tabia ya kulaumu kisha aondolewe tutadumaa hapa hapa kisoka," alisema. Alisema Kim, ni mmoja wa makocha wazuri kutokana na kufanya nae kazi akiwa kama Mkufunzi wa FIFA wa makipa wa timu za taifa za vijana, hivyo aliwataka wadau wa soka wasimbughudhi ili afanye kazi zake kwa ufanisi. Aliongeza, licha ya kuwataka wadau wawe na subira pia wasiweke tumaini kubwa la Tanzania kufuzu fainali zijazo za Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini au Kumbe la Dunia la Brazil, ingawa alikiri lolote linaweza kutokea. "Tukifuzu itakuwa ni bahati, lakini nadhani tunapaswa kuweka nguvu kwa ajili ya fainali za mbele, tumechelewa mno kujipanga hivyo lolote litakalotokea tulichukulie poa na kujipanga zaidi ili tufuzu michuano ijayo," alisema. Tanzania ipo kwenye mbio za kuwania kufuzu fainali za Afrika ikitarajiwa kuvaana na Msumbiji katika mechi ya marudiano Juni 15 baada ya awali kutoka sare. Pia ipo kundi C na timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia katika mbio za kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 zitakazofanyika nchini Brazil, ikianza kibarua Juni 2 kwa kuumana na Ivory Coast.

No comments:

Post a Comment