STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 12, 2011

Vijana wahimizwa kujifunza uongozi, ujasiriamali

VIJANA wa Kitanzania wamehimizwa kujitosa kwenye masuala ya uongozi na ujasiriamali kwa lengo la kuja kuwa tegemeo la taifa hapo baadae.
Wito huo umetolewa na uongozi wa Chuo cha Viongozi wa Afrika, African Leadership Academy (ALA), kilichopo Afrika Kusini wakati wakitangaza ofa maalum ya kuwasomesha kwa muda wa miaka miwili bure wahitimu wa sekondari na vijana wa Kitanzania.
Mkurugenzi wa Usajili wa chuo hicho, Ivy Mwai, amesema kutokana na hali ilivyo duniani kwa sasa ni vema vijana wakajifunza masuala ya uongozi na ujasiriamali ili kuweza kujisaidia wenyewe na nchi yao kwa ujumla.
Mwai alisema vijana wenye ndoto za kuwa viongozi au wajasiriamali ni lazima wajisomee fani hizo kisha kujitokeza bila hofu yoyote kwa lengo la kuiletea nchi maendeleo.
"Vijana wa Kitanzania wenye vipaji vya uongozi na ndoto za kuwa wajasiriamali wajitokeze hadharani ili wapate ujuzi na uzoefu kwa manufaa ya taifa hapo baadae," alisema Mwai.
Mwai, alisema kutokana na kupenda kuona nchi za kiafrika zinapiga hatua kubwa kimaendeleo chuo chao kimetoa ofa Tanzania kwa kuwasomesha watakaojisajili na kufuzu kwenye mchujo utakaofanyika Mei mwaka huu.
Alisema usajili wa wahitimu hao wa sekondari na vijana wenye sifa utaanza kufanyika kuanzia mwezi ujao na watakaoshinda watatangazwa Mei kabla ya kwenda kujiunga na chuo hicho.
"Lengo letu ni kutaka kuona Tanzania na nchi za Kiafrika zinakuwa na viongozi wenye uchungu wa kuziletea mabadiliko nchi yao kimaendeleo na hivyo tumeamua kutoa ofa maalum kwa vijana wa hapa," alisema.
Mwai alisema kijana yeyote mwenye umri kati ya miaka 16-19 wanaweza kuichangamkia ofa hiyo itakayoambatana na kusaidiwa kutafutiwa vyuo vikuu vya kimataifa pale watakapofanya vema kwenye masomo yao ALA kwa kujaza fomu kupitia barua pepe admissions@africanleadershipacademy.org.
Mmoja wa wanafunzi wa Kitanzania aliyewahi kupata ofa kama hiyo ya ALA, Julius Shirima, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Chama cha Wajasiriamlia Mkoa wa Dar es Salaam, DARECHA, alisema vijana hawapaswi kuipoteza bahati hiyo.

No comments:

Post a Comment