STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, June 7, 2012

Bingwa wa karate aililia serikali

BINGWA wa mchezo wa Karate kwa nchi za Afrika Mashariki ngazi ya klabu, Sensei Mikidadi Kilindo, ameiomba serikali iutupie macho mchezo huo na kuupa sapoti kama ilivyo kwa michezo mingine ili kuuhamasisha nchini. Aidha, Kilindo amedai kuwa kutopewa kipaumbele kwa mchezo huo ndio kilichomfanya mara zote awe anaenda na kurudi na medali bila hata kutangazwa au kufahamika kwa wananchi kitu kinachomsikitisha. Akizungumza na MICHARAZO , Sensei Kilindo alisema licha ya mchezo huo kuwa na manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla umekuwa haupewi kipaumbele kama michezo mingine. Alisema kutokana na hali hiyo ni vema serikali na wadau wa michezo kuutupia macho na kuusaidia ili utangazike na kutumiwa kuiletea sifa Tanzania baada ya michezo mingine kushindwa kufanya hivyo. Bingwa huyo wa miaka minne mfululizo wa Afrika Mashariki tangu 2008 alisema, kutopewa kipaumbele kwa karate ndiko kunakofanya hata wachezaji wanaoenda kuitangaza nchi wasifahamike warudipo na ushindi. "Mimi nimerudi hivi karibuni na medali ya dhahabu baada ya kuwa mshindi wa kwanza Afrika Mashariki, hii ni mara ya nne mfululizo, ila hakuna anayejua wala kiongozi aliyewahi kunipokea na kunipongeza inauma sana," alisema. Pia Kilindo alisema ukimya unaofanywa na viongozi wa Chama cha Karate nchini, TASHOKA katika kuutangaza mchezo huo ni tatizo linalofanya usisikike licha ya mafanikio yake kwa ngazi ya klabu. Alisema ni vema TASHOKA ikafanya utaratibu wa kuandaa michuano ya taifa angalau mara mbili kwa mwaka itakayoshirikisha klabu mbalimbali nchini kwa lengo la kuuhamasisha na kuutangaza mchezo huo.

No comments:

Post a Comment