STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, September 29, 2012

TFF YATOA ITC NNE, VODACOM, KLABU ZAMALIZANA  LIGI KUU 



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanne waliokuwa wakichezea timu mbalimbali nchini.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema jana jijini kuwa, wachezaji hao ni Tony Ndolo aliyejiunga na KCC ya Uganda kutoka Toto Africans, Felix Amech Stanley aliyekwenda Bahla ya Oman kutoka Coastal Union, Ernest Boakye kutoka Yanga aliyejiunga na Tripoli Athletics Club ya Lebanon na Derrick Walulya aliyerejea URA ya Uganda kutoka Simba.
Katika hatua nyingine, Wambura amesema wanamichezo 15 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) utakaofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao.
Aliwataja waliochukua fomu za kuwania uenyekiti ni Lina Kessy, Isabellah Kapera na Joan Minja. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti imeombwa na Roseleen Kisiwa pekee wakati Katibu Mkuu ni Amina Karuma na Cecilia Makafu. Macky Mhango pia ni mwombaji pekee aliyeomba nafasi ya Katibu Msaidizi.
Alisema waombaji watatu wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni Furaha Francis, Juliet Mndeme na Zena Chande. Nafasi ya Mhazini nayo ina mwombaji mmoja tu ambaye ni Rose Msamila.
Alisema Sophia Charles, Rahim Maguza, Telephonia Temba na Jasmin Badar Soud wao wanaomba nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho kwenye uchaguzi huo ambao utaendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya Ombeni Zavalla.
Wakati huo huo: Klabu za Ligi Kuu na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom zimekutana jana mjini Dar es Salaam.
Wambura amesema mazungumzo yalilenga kipengele ya upekee (exclusivity) kilichopo kwenye mkataba wa udhamini ambacho kitaendelea kuwepo. Klabu zilikuwa zimeomba kwa mdhamini kuangalia uwezekano wa kukiondoa.
Alisema pande hizo zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kuitafutia kila klabu mdhamini binafsi kwa lengo la kuhakikisha zinashiriki kikamilifu katika ligi hiyo na kwamba klabu zote zimeshapata vifaa kutoka kwa Vodacom ukiondoa African Lyon ambayo ilitarajia kuchukua vifaa hivyo leo kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo.
Kuhusu mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Soka Tanzania (TAFCA), Wambura alisema unaanza rasmi Septemba 30 mwaka huu kwa uchukuaji fomu kwa wagombea.
Alisema kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, fomu kwa waombaji uongozi zitaanza kutolewa Septemba 30 mwaka huu, na mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ni Oktoba 4 mwaka huu.
Alisema fomu hizo zinapatikana ofisi za TAFCA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 alasiri. Ada ya fomu kwa waombaji wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi ni sh. 200,000.
Alisema nafasi zilizobaki za Mweka Hazina, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ada ya fomu ni sh. 100,000. Uchaguzi wa TAFCA umepangwa kufanyika Novemba 10 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment