STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, November 10, 2012

AGGREY MORRIS NAYE ATIMULIWA AZAM 

Aggrey Morris (kushoto) aliyesimamishwa na timu yake ya Azam


BEKI wa Azam FC, Aggrey Morris Ambroce amefukuzwa kwenye kambi ya timu hiyo leo mjini Tanga, baada ya kuthibitika naye alipokea rushwa kutoka klabu ya Simba ili kuihujumu timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Aggrey ameondolewa kambini leo, siku moja tu baada ya kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Said Mourad na Erasto Nyoni nao kusimamishwa kwa tuhuma hizo.
Azam ilifungwa na Simba mabao 3-1 Oktoba 27, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi za Ligi Kuu na baada ya hapo ikamfukuza kocha wake Mserbia, Boris Bunjak na kumrejesha Muingereza, Stewart Hall.
Habari kutoka ndani ya Azam zimesema kwamba baada ya kupata taarifa hizo, uongozi ulizifanyia kazi taratibu na kujiridhisha kabisa wachezaji hao watatu walikula njama za kuihujumu timu katika mechi hiyo.
Kwa sababu hiyo, uongozi kwanza umewasimamisha wachezaji hao na hatua zaidi zitafuatia baadaye.
Hata hivyo, Dida hakucheza mechi hiyo, kwani Oktoba 27, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz aliyempisha Abdi Kassim, Himid Mao aliyempisha Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Herman Tcheche na Salum Abubakar.
Siku hiyo, Azam walitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja, kabla ya Felix Mumba Sunzu Jr., kuisawazishia Simba dakika mbili baadaye, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
Okwi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto na dakika tano tu tangu kuanza kipindi cha pili, Mganda huyo tena akawainua vitini mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka mabeki wa Azam.
Habari zaidi zinasema kwamba, uchunguzi unaendelea kufanywa juu ya wachezaji wengine wanaotuhumiwa kuwa katika mkumbo huo wa kuihujumu timu na ikithibitika ni ukweli, watachukuliwa hatua pia bila kujali majina yao.
Azam tayari iko Tanga tangu jana saa 8:00 mchana wa kwa ajili yao ya mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho dhidi ya Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani.

No comments:

Post a Comment